Madrid yashikilia hatma ya Hispania, Arsenal ndo hivyo

Muktasari:

  • Madrid ndio imeshikilia hatma ya Hispania kwani ikitolewa leo, rasmi Hispania itakuwa imeshindwa kuingiza timu katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2019-20.

BAADA ya timu mbili za Hispania, Barcelona na Atletico Madrid kuaga rasmi michuano ya Ligi ya Mabingwa jana, leo Real Madrid itakuwa imeshikilia hatma ya Hispania ya kuingiza timu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Barcelona ilitolewa na Paris Saint-Germain kwa kipigo cha jumla cha mabao 6-4, ambapo mchezo wa kwanza kule Ufaransa iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 kisha marudiano pale Hispania jana ikafungwa mabao 4-1 baada ya beki wao Ronald Araujo kutolewa kwa kadi nyekundu mapema katika dakika ya 29 wakati wakiongoza 1-0 kwa bao la Raphinha kabla ya winga wao wa zamani, Ousmanne Dembele kusawazisha, Vitinha akaweka jingine na Kylian Mbappe akatupia mawili likiwamo la penalti ya dakika ya 89.

Kwa upande wa Atletico ilitolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 6-3, mchezo wa kwanza kule Hispania ikishinda 2-1 na marudiano Ujerumani ikaambulia kichapo cha mabao 4-2.

Leo, Madrid itakuwa pale Engaland kucheza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City.

Mechi hii ya mkondo wa pili itakuwa ni ya lazima kwa Madrid kushinda ili kusonga mbele kwani mechi ya kwanza ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3 na hamna sheria ya bao la ugenini.
Madrid ndio imeshikilia hatma ya Hispania kwani ikitolewa leo, rasmi Hispania itakuwa imeshindwa kuingiza timu katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2019-20.

Mchezo huu unatarajiwa kupigwa katika dimba la Etihad kuanzia saa 4:00 usiku.

Arsenal ambayo imerudi katika hatua hii kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2009-10, itakuwa na kazi ya kufuzu nusu fainali yao ya kwanza tangu mwaka 2006.

Arsenal itakutana na Bayern Munich nchini kwenye uwanja wa Allianz Arena katika mchezo ambao utaanza saa 4:00 usiku.
Mechi ya kwanza iliyopigwa pale Emirates Studium ilimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2.