Madrid yachomoa kwa Van Dijk
Muktasari:
- Van Dijk anajiandaa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu endapo kama hatasaini mkataba mpya kwenye kikosi chake cha Liverpool kwa sasa, ambako dili lake litafika ukomo Juni, mwaka huu.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeripotiwa kwamba imepiga chini mpango wa kumsajili beki wa Liverpool, Virgil van Dijk baada ya wakala wa Mdachi huyo kumtoa ofa kwa wababe hao wa La Liga.
Van Dijk anajiandaa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu endapo kama hatasaini mkataba mpya kwenye kikosi chake cha Liverpool kwa sasa, ambako dili lake litafika ukomo Juni, mwaka huu.
Van Dijk, 33, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Liverpool tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Southampton, Januari 2018, aliisaidia miamba hiyo ya Anfield kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England.
Lakini, sasa staa huyo yupo kwenye hatari ya kuondoka bure klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu kama Liverpool itashindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya, kitu ambacho miamba hiyo ya Anfield inaweza kuwapoteza bure pia wachezaji Mohamed Salah na Trent Alexander-Arnold, ambao pia mikataba yao itamalizika mwishoni mwa msimu.
Kinachoripotiwa ni kwamba wakala wa Van Dijk alimtoa ofa beki huyo wa Kidachi kwenda Real Madrid kwa uhamisho wa bure kwa maana ya kuhakikisha inamsainisha mkataba wa awali kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Wakala huyo anaamini shida ya majeruhi wengi wa nafasi ya mabeki kwenye kikosi cha Los Blancos akiwamo David Alaba na Eder Militao itampa dili mteja wake.
Van Dijk si mchezaji pekee wa Liverpool anayehusishwa na Real Madrid kwa sababu Alexander-Arnold naye yupo kwenye rada za miamba hiyo inayolewa na Mtaliano Carlo Ancelotti na imeelezwa ofa yao ya kwanza iligomewa huko Anfield.