Madrid mmh! Ancelotti ni matatizo

Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Goal.com, inaelezwa kocha wa Madrid, Carlo Ancelotti haelewani na kocha wa viungo wa timu hiyo, Antonio Pintus.
MADRID, HISPANIA: WAKATI taarifa za mpasuko baina ya mastaa wa Real Madrid zikizidi kupamba moto, inaripotiwa hata benchi la ufundi nalo mambo hayaeleweki.
Kwa mujibu wa tovuti ya Goal.com, inaelezwa kocha wa Madrid, Carlo Ancelotti haelewani na kocha wa viungo wa timu hiyo, Antonio Pintus.
Real Madrid iliuanza msimu vibaya tofauti na ilivyotarajiwa licha ya kukamilisha uhamisho wa Kylian Mbappe ambaye ilionekana ni kama Cristiano Ronaldo mpya, lakini kila uchao imekuwa ikipata matokeo mabaya huku taarifa zikidai kuwa Ancelotti amekalia kuti kavu.
Hata hivyo, moja kati ya mambo yanayoripotiwa kuiumiza timu hiyo ni majeruhi ambapo kwa msimu huu ndani ya miezi mitatu wamefikia 25.
Kwa sasa Ancelotti ana wachezaji tisa majeruhi akiwemo David Alaba, Joan Martinez, Dani Carvajal, Jacobo Ramon, Eder Militao, Thibaut Courtois, Aurelien Tchouameni, Lucas Vazquez na Rodrygo.
Kwa mujibu wa The Athletic, hali hiyo imesababisha Ancelotti kutokuwa na imani na makocha wa viungo kuhusu maandalizi ya kimwili ya timu.
Pintus inaelezwa wachezaji wamekuwa wakimkosoa kutokana na aina ya mazoezi anayowapa na mwaka jana Jude Bellingham alikaririwa akisema, "kocha huyo anapenda kututesa."
Hata hivyo, vyanzo vya karibu na kocha huyo vinaeleza kuwa Pintus anaamini ratiba nzito ya timu ndicho chanzo cha majeruhi kuongezeka.
Inaripotiwa kwamba uhusiano wa Pintus na Ancelotti ulianza kuingia dosari miezi ya hivi karibuni.
Ancelotti anaamini tatizo la majaruhi linasababishwa na uzembe wa Pintus ambaye yupo katika hatihati ya kufukuzwa kwani kocha huyo mkuu hamwamini tena.