Mabosi Saudi Arabia hawajamkatia tamaa Mo Salah
Muktasari:
- Mo Salah amepitia kipindi chenye misukosuko akiwa Liverpool chini ya kocha Arne Slot na ingawa uhamisho mwezi huu hauwezekani tena, uamuzi kuhusu mustakabali wake utafanyika mwishoni mwa msimu.
LIVERPOOL, ENGLAND: MABOSI wenye ushawishi mkubwa katika soka la Saudi Arabia wanaendelea kuamini kwa kiwango kikubwa Mohamed Salah ataondoka Liverpool katika dirisha la usajili la majira ya joto.
Mo Salah amepitia kipindi chenye misukosuko akiwa Liverpool chini ya kocha Arne Slot na ingawa uhamisho mwezi huu hauwezekani tena, uamuzi kuhusu mustakabali wake utafanyika mwishoni mwa msimu.
Kwa muda mrefu Salah amekuwa akihusishwa na uhamisho wa pesa nyingi kwenda Saudi Arabia na uvumi uliongezeka mwezi Desemba baada ya yeye kuingia kwenye mgogoro wa wazi na kocha Slot.
Mmisri huyo alimtuhumu Slot kwa kumtupia lawama hadharani wakati timu ilipokuwa kwenye kiwango kibaya, jambo lililofanya uwezekano wa kuondoka Januari uonekane mkubwa.
Hata hivyo, muda ambao Salah alikuwa nje ya Liverpool akichezea Misri kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) uliwapa pande zote mbili nafasi ya kutafakari misimamo yao, na hali sasa imetulia.
Salah alirejea moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza katika ushindi wa Liverpool wa mabao 3-0 dhidi ya Marseille kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano iliyopita na mambo yameanza kutengamaa.
Msisimko wa usajili mkubwa katika soka la Saudi Arabia unaonyesha dalili za kupungua, huku baadhi ya nyota waliovutwa kutoka ligi kubwa za Ulaya sasa wakitaka kurejea.
Lakini Salah ana hadhi ya kipekee kabisa kama mchezaji kutokana na imani yake na klabu kubwa za Saudia bado zinaendelea kuvutiwa naye.
Gazeti la The i Paper limemnukuu chanzo kutoka Saudi Arabia kikisema uhamisho wa Salah kutoka Liverpool kwenda Saudi Pro League katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi “hauepukiki”. Hapo awali iliripotiwa Al-Hilal, Al-Qadisiyah na Neom zilikuwa zikimtaka Salah, huku mkuu wa Ligi Kuu Saudi, Omar Mugharbel, akitangaza hadharani kuwa Salah anakaribishwa kwenye ligi hiyo.
Gazeti la The Telegraph limeripoti kuwa Salah na nyota wa Real Madrid, Vinícius Júnior, ndiyo malengo makuu mawili ya ligi hiyo, huku Sadio Mané, Fabinho, N’Golo Kanté na Karim Benzema wakitajwa huenda wakaondoka mwaka huu. Kuna hisia Saudi Pro League italazimika kufanya usajili mkubwa wa kuvutia majira ya joto ili kudumisha kasi yake.
Hisia hizo zitaongezeka zaidi iwapo Kante na Ruben Neves wataondoka Saudi Arabia mwezi huu. Kiungo wa zamani wa Chelsea, Kante, yuko kwenye mazungumzo ya kujiunga na Fenerbahce kutoka Al-Ittihad, huku Neves, aliyewahi kucheza Wolves, akihusishwa na Manchester United na klabu nyingine.
Wakati huo huo, Saud Pro League inafahamu pia ushindani kutoka Ligi ya Nyota ya Qatar, ambayo tayari imefanikiwa kuwavutia Roberto Firmino, Marco Verratti na Julian Draxler.
Salah bado ana mkataba na Liverpool hadi Juni 2027, baada ya kusaini dili jipya la mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki mwishoni mwa msimu uliopita.
Liverpool ilikataa ofa ya Pauni 150 milioni kutoka Al-Ittihad Septemba 2023 na mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza kuwa haendipopote, huku Slot akimsifu sana kwa taaluma yake baada ya ushindi dhidi ya Marseille.
Slot amesema: “Inaonyesha ni mtaalamu mkubwa kiasi gani kuwa anaweza kuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja akiwa na timu tofauti, halafu akarudi akiwa fiti kucheza dakika 90 baada ya siku moja tu ya mazoezi. Alikuwa karibu sana kufunga bao. Kwa kawaida angefunga, lakini haikutuumiza kwa sababu tulifunga mabao matatu.”