Mabao ya Palmer hayana hela

LONDON, ENGLAND. MTAMBO wa mabao wa Chelsea, Cole Palmer ameripotiwa hakuna pesa yoyote anayopata kama bonasi kutokana na kasi yake ya kutikisa nyavu za wapinzani kwa msimu huu.
 

Palmer aliyesajiliwa na Chelsea kwa ada ya Pauni 42.5 milioni dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ameshafunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England na kulingana na straika wa Manchester City, Erling Haaland kwenye mbio za kusaka Kiatu cha Dhahabu kwenye ligi hiyo msimu huu.
 

Hata hivyo, Palmer, 21, alidai wala hajali hakuna kipengele chochote kinachofichua atalipwa bonasi kutoka kwenye mshahara wake wa Pauni 80,000 kwa wiki anaolipwa huko Stamford Bridge kutokana na kufunga mabao mara nyingi.

Anachojivunia ni kuingia kwenye rekodi zake binafasi na kwa kitendo chake cha kufunga mabao manne kwenye ushindi wa 6-0 iliyopata Chelsea dhidi ya Everton, Jumatatu iliyopita, imemfanya kuwa mchezaji wa 40 kufunga mabao manne kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England.
Ilikuwa mara ya kwanza pia mchezaji mmoja kufunga mabao manne katika mechi moja tangu Kevin de Bruyne alipofanya hivyo dhidi ya Wolves, Mei 2022.
 

Si kwenye hilo tu, Palmer pia aliweka rekodi ya kufunga hat-trick sahihi zaidi kwenye kipindi cha kwanza na bao la kwanza alifunga kwa mguu wa kushoto, la pili kwa kichwa na la tatu kwa mguu wa kulia alipouchopu mpira kiufundi. Jambo hilo lilimfanya kuwa mchezaji wa 36 kufunga hat-trick ya aina hiyo kwenye Ligi Kuu England.
 

Kwenye mechi ambayo Palmer alifunga mara nne, bao lake la nne ni la penalti ambalo lilisababisha vurugu baada ya wachezaji wengine wa Chelsea, Noni Madueke na Nicolas Jackson kugombea mpira wakitaka wapige hao, kabla ya nahodha Conor Gallagher kuingilia kati na kumwacha kiungo huyo mchezeshaji Mwingereza apige mkwaju huo.