Maajabu ya siku 475 za nyota wa Marekani, Alex Freeman
Muktasari:
- Nyota huyo ambaye jina lake kamili ni Alexander Michael Freeman ni mchezaji wa soka wa Marekani aliyezaliwa Agosti 9, 2004, katika mji wa Baltimore uliopo katika jimbo la Maryland, anayecheza nafasi ya beki wa kulia huku akiwa na uwezo pia wa kucheza winga ya kulia kwa ufasaha.
WASHINGTON, MAREKANI: MCHEZAJI nyota wa timu ya taifa ya Marekani, Alex Freeman amekuwa na siku 475, zilizojaa historia maishani mwake baada ya leo kufunga bao lake la kwanza la Kombe la Dunia, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Australia.
Nyota huyo ambaye jina lake kamili ni Alexander Michael Freeman ni mchezaji wa soka wa Marekani aliyezaliwa Agosti 9, 2004, katika mji wa Baltimore uliopo katika jimbo la Maryland, anayecheza nafasi ya beki wa kulia huku akiwa na uwezo pia wa kucheza winga ya kulia kwa ufasaha.
Alex alianza kuitwa timu ya taifa ya Marekani rasmi mwaka 2025, baada ya kushiriki michuano ya Gold Cup ya mwaka 2025, akiwa ni miongoni mwa nyota waliotabiriwa makubwa zaidi.
Mwanzo wa maisha yake nyota huyo alikulia Florida, ambako alianza kucheza soka akiwa na umri mdogo akipitia akademi za vijana za Weston FC Academy na Orlando City Academy akionyesha kipaji bora cha kuvutia.
Baba yake anayejulikana kwa jina la Antonio Freeman, alikuwa mchezaji wa National Football League (NFL) na mshindi wa fainali ya Super Bowl huko Marekani inayovuta hisia zaidi za mashabiki wanaovutiwa na mchezo huo.
Mwaka 2022, Alex alisaini mkataba na Orlando City akiwa ni mchezaji wa akademi baada ya mwanzo kucheza zaidi timu za vijana ya Orlando City B na kuendelea kuonyesha kipaji kizuri.
Nyota ya mchezaji huyo ilianza rasmi kung'aa Machi 1, 2025, ambapo hadi leo hii ni sawa na siku 475, akiwa ni miongoni wa vijana wenye vipaji vya kuvutia kutokana na uwezo alionao.
Machi 1, 2025, ilikuwa siku ya historia kwa nyota huyo baada ya kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), akiwa na kikosi hicho cha Orlando City na kuendeleza makali yake yanayochagiza umuhimu wake.
Oktoba 30, 2025, Alex alishinda tuzo ya mwaka ya mchezaji bora kijana wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS Young Player of the Year 2025) kutokana na kuonyesha kiwango bora cha kuvutia.
Tuzo hiyo aliipata akiwa na Orlando City, akihusika na mabao tisa ya kikosi hicho baada ya kufunga sita na kutoa asisti tatu katika mechi 29, alizocheza ikiwa ni kiwango bora kwa mchezaji anayecheza nafasi ya beki uwanjani.
Ubora wa kipaji chake uliendelea kuonekana baada ya Januari 29, 2026, nyota huyo kusajiliwa na Klabu ya Villarreal CF inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) kutokana na maskauti wa kikosi hicho kuvutiwa na kipaji chake.
Juni 19, 2026, nyota huyo akaandika rekodi nyingine mpya ya kufunga bao lake la kwanza katika Kombe la Dunia, katika ushindi wa Marekani wa mabao 2-0, dhidi ya Australia na kutumia siku 475 za maajabu tangu mchezaji huyo alipoanza rasmi kung'aa Machi 1, 2025.