Luis Enrique: Anfield itatujua

Muktasari:
- Kocha huyo wa miamba ya Ligue 1, Enrique alihuzunishwa na matokeo iliyopata timu yake kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo bao la mchezaji Harvey Elliott alilofunga kwenye dakika 87 lilitosha kuipa Liverpool ushindi wa 1-0 ugenini.
PARIS, UFARANSA: KOCHA wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique ameionya Liverpool kwamba vijana wake watakuwa hatari zaidi uwanjani Anfield.
Kocha huyo wa miamba ya Ligue 1, Enrique alihuzunishwa na matokeo iliyopata timu yake kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo bao la mchezaji Harvey Elliott alilofunga kwenye dakika 87 lilitosha kuipa Liverpool ushindi wa 1-0 ugenini.
Katika mchezo huo, kikwazo cha PSG kutikisa nyavu kilikuwa kipa wa Liverpool, Alisson Becker, ambaye aliokoa hatari tisa na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Na sasa miamba hiyo ya Ufaransa itasafiri kwenda Anfield wiki ijayo kwenye mechi ya marudiano ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kocha Enrique alisema: “:Hatuna cha kupoteza na hiyo ni hatari sana.”
PSG ingekuwa mbele kwa mabao matatu au manne hadi mapumziko, lakini kipa Alisson alikuwa kwenye kiwango bora alipowagomea Ousmane Dembele, Bradley Barcola na Khvicha Kvaratskhelia katika kipindi cha kwanza. Vinara hao wa Ligue 1 walikuwa kwenye rekodi ya kucheza mechi 22 bila kupoteza na ilikuwa imefunga mabao 40 katika mechi 10 zilizopita.
Enrique aliongeza: “Ni ngumu sana kufikiria ile mechi katika mtazamo chanya. Tulistahili kushinda. Mchezaji bora wa Liverpool alikuwa kipa wao. Soka kuna muda halitendi haki.
“Hatuna cha kupoteza na tupo tayari kwa kipute cha Liverpool. Tunakwenda kumaliza.”
Kipa Alisson alisifu kiwango chake katika mechi hiyo, aliposema: “Nilikuwa kwenye kiwango bora kabisa cha maisha yangu. Kocha alituambia ni ngumu kiasi gani kwenda kucheza dhidi ya PSG, ni wazuri sana kwenye mpira na kwamba tulipaswa kujiandaa kwenye kutaabika. Tulijua hicho kitakwenda kutokea. Kwa jitihada za wengine walinisaidia kufanya kazi yangu. Kisha Harvey (Elliott) aliingia na kufunga bao, ilikuwa hadithi nzuri kwetu. Usiku bora kabisa.”