Liverpool yahamia kwa Osimhen

Muktasari:
- Kocha, Arne Slot anataka huduma ya straika mpya kwenye kikosi chake baada ya kutokuwa na uhakika na hatima ya mshambuliaji, Darwin Nunez.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imemwongeza Victor Osimhen kwenye orodha ya mastraika inaowasaka kwa ajili ya kuwaongeza kwenye kikosi msimu huu sambamba na Alexander Isak na Hugo Ekitike.
Kocha, Arne Slot anataka huduma ya straika mpya kwenye kikosi chake baada ya kutokuwa na uhakika na hatima ya mshambuliaji, Darwin Nunez.
Staa huyo wa Uruguay, Nunez anahusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na mabingwa wa Serie A, Napoli. Na kama ataondoka, basi mchezaji wa kuja kuchukua mikoba yake ni mpango uliopo mezani Liverpool.
Na kwenye hilo, orodha ndefu ya mastraika imewekwa kwenye mipango ya Liverpool ikihitaji huduma ya mmoja kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Straika wa Eintracht Frankfurt, Ekitike ni miongoni mwa wale waliovutia wengi kwa kiwango bora alichokionyesha msimu uliopita huko Ujerumani, lakini sasa itabidi asubiri kiasi kabla ya kutua Anfield.
Hii ni kwasababu, Liverpool itahitaji kuuza wachezaji wake kwanza ili kupata pesa za kusajili. Hiyo ni kwasababu kuna matarajio kwamba Frankfurt itahitaji ilipwa Pauni 85 milioni kwa ajili ya Mfaransa huyo, hasa baada ya bosi wa Frankfurt, Markus Krosche kufichua hawawezi kumuuza staa wao kwa pesa ndogo.
Krosche alisema: “Kama bei haitakuwa sawa, basi atabaki. Hatuwezi kumuza Hugo.â€
Liverpool pia imekuwa ikitazama wachezaji wengi na kwenye hiyo, yupo staa wa Newcastle, Alexander Isak, lakini huduma yake ni ghali zaidi, Pauni 150 milioni. Kutokana na hilo, ndiyo maana mabosi wa Liverpool, wamemwongeza kwenye rada zao, straika wa Napoli, Osimhen, ambaye wanaamini wanaweza kumpata kwa bei ya chini kiasi.
Osimhen alikuwa kwa mkopo Galatasaray msimu uliopita, ambako alifunga mabao 37 na kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachoeleza kwamba saini yake inaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 63 milioni tu.