Lionel Messi: Sina urafiki na Cristiano Ronaldo

Muktasari:
- Messi ambaye kwa sasa anashiriki Fainali za Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Inter Miami, amesema kwamba mazingira yamesababisha yeye na Ronaldo wasiwe na ukaribu japo wanaheshimiana.
Nyota wa Inter Miami na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi (37) amefichua kuwa hana urafiki na staa wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo (40).
Messi ambaye kwa sasa anashiriki Fainali za Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Inter Miami, amesema kwamba mazingira yamesababisha yeye na Ronaldo wasiwe na ukaribu japo wanaheshimiana.
“Ushindani naye (Ronaldo) ulikuwa katika eneo la kuchezea. Kila mmoja wetu alitaka kufanya vizuri zaidi kwa ajili ya timu. Kawaida kama ilivyo mara zote, kila kitu kinabakia uwanjani.
“Nje ya uwanja sisi ni watu wa kawaida. Sio marafiki kikawaida kwa sababu hatutumii muda pamoja lakini kila siku kila mmoja anampa mwenzake heshima kubwa,” amesema Messi.
Kauli ya Messi ni kama marudio ya alichokisema mwaka 2017 kuhusu mahusiano yake na Ronaldo.
“Sijui kama tutakuwa marafiki (na Ronaldo). Urafiki unajengwa kwa kutumia muda pamoja na kupata nafasi ya kufahamiana kila mmoja.
“Hatuna uhusiano kwa sababu tunaonana katika sherehe za tuzo pekee na hapo ndio muda pekee tunaozungumza,” alinukuliwa Messi.
Mapema mwaka huu, Ronaldo alinukuliwa akisema hana shida na Messi.
“Nina mahusiano mazuri na Leo Messi. Nilikuwa namtafsiria Kiingereza katika sherehe za tuzo. Ilifurahisha.
“Ni ushindani wa kiafya ambao tumekuwa nao,” alisema Ronaldo.