Leverkusen kuzibania Bayern, City kwa Wirtz

Muktasari:
- Staa huyu ambaye anahitajika na Bayern Munich na Manchester City, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
BOSI wa Bayer Leverkusen, Fernando Carro anaamini kuna nafasi ya asilimia 50 kwa kiungo wao wa kimataifa wa Ujerumani, Florian Wirtz mwenye umri wa miaka 22, kubakia katika kikosi hicho licha ya kuhusishwa na timu mbalimbali barani Ulaya.
Staa huyu ambaye anahitajika na Bayern Munich na Manchester City, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Wirtz ameshaweka wazi kwamba anatamani kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine lakini itategemea na makubaliano ya mazungumzo baina ya timu yake na timu zinazomhitaji.
Hata hivyo, mabosi wa Leverkusen wanataka kujaribu kumpa fundi huyu mkataba mpya ambao utamshawishi abaki ingawa inaonekana kuwa ngumu.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao 16.
Wirtz amekuwa akiwasha moto mkali hata anapoitumikia timu ya taifa ya Ujerumani.
Leroy Sane
BAYERN Munich haina mpango wa kuboresha ofa yake ya mkataba kwa winga wake wa kimataifa wa Ujerumani, Leroy Sane, licha ya mawakala wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, kuwasilisha pendekezo jipya la mshahara kwa mabingwa hao wa Bundesliga.
Mkataba wa sasa wa Sane unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Sane anahusishwa na mipango ya kuondoka kutokana na kutoridhishwa na ofa ya Bayern.
Kevin de Bruyne
MKURUGENZI wa michezo wa Napoli, Giovanni Manna, bado hajatoa tamko lolote kama wana mpango wa kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin de Bruyne, 33, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
De Bruyne mwenye umri wa miaka 33, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na ameshaaga kuwa anaondoka.
Jakub Kiwior
BEKI wa kati wa Arsenal, Jakub Kiwior yuko kwenye rada ya Juventus na Inter Milan zinazohitaji kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Fundi huyu wa kimataifa wa Poland, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, hadi sasa bado hajafanya uamuzi wa wapi atatua katika dirisha lijalo.
Msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote.
Kelleher
WEST Ham wanataka kumsajili kipa wa Liverpool na wa Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher, mwenye umri wa miaka 26, katika dirisha la majira ya kiangazi.
Kelleher anataka kuondoka Liverpool kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha majogoo hao. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Jonathan David
MSHAMBULIAJI wa Lille na timu ya taifa ya Canada, Jonathan David ambaye atakuwa mchezaji huru mwisho wa msimu huu ni miongoni mwa mastaa wanaowindwa na Napoli inayohitaji kumsajili kaitka dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mbali ya Napoli, staa huyu pia anawindwa na Barcelona ambayo imeshawishika zaidi na kuwa kwake huru.
David Hancko
AC Milan wameonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa Feyenoord, David Hancko katika dirisha lijalo lakini wanakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa Bayer Leverkusen na Juventus amnbazo pia zimeonyesha nia ya kumsajili beki huyo wa kimataifa wa Slovakia mwenye umri wa miaka 27. Hancko ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.
Trent Alexander-Arnold
REAL Madrid wapo tayari kutoa ada ya uhamisho ya Pauni 1 milioni kwenda Liverpool kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa timu hiyo, Trent Alexander-Arnold, 26, mapema ili kumtumia katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu inayotarajiwa kuanza mwezi ujao. Mkataba wa Trent ambaye ameshaweka wazi kwamba ataondoka, unamalizika Juni 30.