Duh! Tajiri wa Forest amvaa kocha uwanjani

Muktasari:
- Marinakis alionekana akizungumza kwa mikono kumwelekea Kocha Espirito Santo, ambaye alionekana kumsogelea bosi huyo na kujaribu kuweka hali ya amani.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Nottingham Forest, Nuno Espirito Santo amesema anazielewa hasira za mmiliki wa klabu hiyo, Evangelos Marinakis baada ya kumvamia uwanjani na kuanza kubwata baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Leicester City kwenye Ligi Kuu England, Jumapili.
Marinakis alionekana akizungumza kwa mikono kumwelekea Kocha Espirito Santo, ambaye alionekana kumsogelea bosi huyo na kujaribu kuweka hali ya amani.
Forest ilikumbana na pigo la kutibua mpango wao wa kufukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini imejiweka kwenye nafasi ya kucheza Europa League kwa sare hiyo.
Kilichoonekana bosi huyo alianza kukasirika tangu mchezaji Taiwo Awoniyi alipoachwa aendelee kucheza wakati aliumia kabla ya kutoka uwanjani na kuifanya timu kubaki na wachezaji 10 uwanjani. Mshambuliaji huyo, Awoniyi aligonga kwenye mwamba wa goli na kuumia, lakini aliendelea kucheza.
Kocha Espirito Santo alisema amezielewa hasira za bosi wake, alisema: “Soka ni mchezo wa hisia, inakuwa ngumu kujizuia pindi unapokuwa na matarajio makubwa.”
“Mashabiki wetu walikuwa vizuri, tulitaka kuendeleza mapambano. Nafasi haipo kwenye mikono yetu, tunapongeza jitihada za kila mchezaji na mashbiki wetu. Haipo kwenye mikono yetu, lakini haijaisha.”
Hasira za tajiri Marinakis zilikuja baada ya kocha kumwacha Awoniyi uwanjani, kwa sababu bosi alitaka aingie mchezaji mwingine mwenye nguvu ambaye angefunga bao na kuipa timu ushindi.
“Tulifanya mabadiliko, kisha tukacheza tukiwa pungufu. Hilo ni lazima likupe hasira, inaeleweka,” alisema Espirito Santo. Bosi huyo wa Marinakis ndiye pia anayeimiliki klabu ya Olympiakos ya Ugiriki.