Kwa hawa Halaand, Ronaldo wanasubiri
Muktasari:
- Julian Quinones ana msimu wa kipekee akiwa na Al-Qadisiya ya Ligi Kuu Saudi Arabia (Pro League) akiwa amefunga mabao 26 akishika nafasi ya pili katika mbio za wafungaji bora duniani kwa sasa.
MEXICO CITY, MEXICO: WASHAMBULIAJI wawili wa Mexico wapo katika viwango vya juu zaidi vya mafanikio uwanjani ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 wakiyazidi mabao baadhi ya majina makubwa duniani wakiwemo Erling Haaland, Kylian Mbappe na Cristiano Ronaldo.
Julian Quinones ana msimu wa kipekee akiwa na Al-Qadisiya ya Ligi Kuu Saudi Arabia (Pro League) akiwa amefunga mabao 26 akishika nafasi ya pili katika mbio za wafungaji bora duniani kwa sasa.
Ni Harry Kane pekee mwenye mabao mengi zaidi (31) kwa sasa kama kinara wa Kiatu cha Dhahabu Ulaya. Naye Armando Gonzalez anaendelea kung’ara ambapo mshambuliaji huyo wa Chivas Guadalajara ya Mexico amefikisha mabao 24 baada ya kufunga mawili dhidi ya Pumas majuzi na kuingia kwenye orodha ya juu ya wafungaji wanne bora duniani.
Gonzalez tayari amewahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Apertura 2025 na ameongeza mabao mengine 12 katika mashindano yanayoendelea. Anaongoza pia orodha ya wafungaji wa Liga MX huku zikiwa zimesalia mechi nne kabla ya msimu kumalizika.
Kinachofanya mafanikio ya mastaa hao wa Mexico kuwa ya kuvutia zaidi ni majina waliyoyaacha nyuma kama Kylian Mbappe na Cristiano Ronaldo ambao wana mabao 23 kila mmoja, huku Erling Haaland akiwa na 22.
Cha kushangaza zaidi siyo Quinones wala Gonzalez ana uhakika wa kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Mexico kwa ajili ya Kombe la Dunia, lakini uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa kocha mkuu Javier Aguirre.