Kumbe Foden anafikiria kuvua samaki
Muktasari:
- Foden amekuwa mmoja wa wachezaji wanaofanya vyema kwenye Ligi Kuu England akiibukia kwenye akademia ya Man City.
MANCHESTER,ENGLAND: STAA wa Manchester City, Phil Foden anataka kutumia muda wake kwenye uvuaji wa samaki wakati atakapostaafu soka.
Foden amekuwa mmoja wa wachezaji wanaofanya vyema kwenye Ligi Kuu England akiibukia kwenye akademia ya Man City.
Akiwa na umri wa miaka 24, tayari ameshashinda mataji sita ya Ligi Kuu England na alikuwa na mchango muhimu wakati Man City iliposhinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023.
Licha ya kwamba bado ana miaka mingi kufikia umri wa kustaafu, Foden tayari ameshafahamu kitu cha kufanya. Alisema atakuwa mwenye furaha kama atatumia sehemu ya maisha yake kwenye kazi za uvuvi wa samaki atakapostaafu soka.
Foden alisema: “Huyu ni mimi nitakapostaafu. Kuwa mvuvi wa samaki. Nilikuwa na umri wa miaka mitano kuna babu mmoja alikuwa akinichukua na kwenda kuvua samaki, basi tangu wakati huo nimejikuta nikipenda kazi hiyo. Nilikuwa navua samaki wa aina tofauti, wadogo na wakubwa.”
Msimu uliopita Foden alikuwa kwenye kiwango matata kabisa akifunga mabao 27 kikosi cha Man City na kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Mwaka, lakini msimu huu staa huyo bado hajaonyesha makali ya kutisha, akifunga bao lake la kwanza kwenye mechi aliyoanzishwa usiku wa juzi Jumanne kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Slovan Bratislava, ambapo Man City ilishinda 4-0. Mabao mengine yalifungwa na Ilkay Gundogan, Erling Haaland na James McAtee, aliyetokea benchini kuja kuchukua nafasi ya straika Haaland.