Kounde, Balde waiwahi Atletico Madrid
Muktasari:
- Wachezaji hao ni Jules Kounde, Alejandro Balde na Frenkie de Jong.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA wa Barcelona, Hansi Flick anatarajiwa kuwa na machaguo zaidi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Hispania dhidi Atletico Madrid kufuatia urejeo wa baadhi ya wachezaji wake ambao walikuwa majeruhi.
Wachezaji hao ni Jules Kounde, Alejandro Balde na Frenkie de Jong.
Kounde na Balde tayari wamerudi mazoezini chini ya Flick na wanatarajiwa kuwa tayari kucheza kwenye mechi ijayo ya La Liga dhidi ya Atletico wikiendi.
Habari hii ni faraja kubwa kwa Flick, kwani itampa chaguo zaidi katika safu ya ulinzi wakati timu inaingia kwenye ratiba ngumu.
Kwa upande wa De Jong, bado yuko nyuma kidogo, hivyo hatarajiwi kuwa tayari kwa mechi ya wikendi. Hata hivyo, ana matumaini ya kurejea kwa wakati ili kucheza mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya haohao, Atletico Madrid.
Katika kipindi ambacho De Jong alikuwa majeruhi, mchezaji Marc Bernal alifanya kazi nzuri kuziba nafasi yake lakini anaweza kupoteza nafasi hiyo mara tu De Jong atakapokuwa fiti.
Pia, Eric Garcia anatarajiwa kuwa amepona kabisa kufikia kurejea kwa ligi, hali itakayoifanya Barcelona ibaki na wachezaji wachache tu majeruhi.
Kwa sasa, waliobaki nje kutokana na majeraha ni Raphinha na Andreas Christensen.