Kosa kubwa la Golden State Warriors dirisha la usajili NBA 2026
Muktasari:
- Hata hivyo, hatua walizochukua huenda zimekuwa miongoni mwa makosa makubwa zaidi ya kimkakati kwa klabu hiyo katika miaka ya karibuni.
GOLDEN State Warriors wamefika siku ya mwisho ya dirisha la usajili katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) 2026 wakiwa njiapanda wakijaribu kusawazisha ili kuwa bora kiushindani sambamba na maandalizi ya maisha baada ya Stephen Curry.
Hata hivyo, hatua walizochukua huenda zimekuwa miongoni mwa makosa makubwa zaidi ya kimkakati kwa klabu hiyo katika miaka ya karibuni.
Kwa muda mrefu, Warriors wamejijengea sifa ya kufanya uamuzi wa kishujaa wakiwa na nasaba iliyotawaliwa na Curry na kubadilisha kikosi bila kusita kila wanapohitaji taji. Lakini, safari hii, mambo yanaonekana kwenda ndivyo sivyo kukionekana migongano na wakati mwingine afya za wachezaji na thamani halisi ya rasilimali walizonazo kuwasumbua.
Msimu wa misukosuko
Warriors wanaingia katika hatua ya mwisho ya msimu wa 2025/26 wakiwa na rekodi ya ushindi 28 na vipigo 24, wakishika nafasi ya nane katika Kanda ya Mashariki yenye ushindani mkali. Mwanzo wa msimu ulikuwa na matumaini, hasa baada ya Jimmy Butler kuingiza uzoefu, ubora katika ulinzi na wastani wa pointi 20 kwa kila mchezo aliocheza.
Lakini, matumaini hayo yalifutika Januari 19 pale Butler alipoumia goti na kumaliza msimu mapema. Pigo hilo limeambatana na maumivu ya goti la kulia yanayomsumbua Curry yakiwaacha Warriors wakipambana kuingia 'play-in' badala ya kupigania nafasi za juu. Mzigo ukaongezeka kwa Draymond Green, huku vijana kama Brandin Podziemski na Moses Moody wakipewa majukumu makubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Dau la dirisha la usajili
Katika jitihada za kuokoa msimu, uongozi wa Warriors ulifanya uamuzi ulioibua mjadala mkubwa - kumtoa Jonathan Kuminga na Buddy Hield kwenda Atlanta Hawks na kumpata Kristaps Porzingis. Pia Trayce Jackson-Davis alihamishwa Toronto Raptors kwa chaguo la raundi ya pili ya drafti.
Kwa makaratasi, Porzingis anaonekana suluhisho kamili akiwa ni mrefu, anayelinda na anaweza kufanya mitupo ya mbali. Lakini, uamuzi huo uliashiria mwisho wa mkakati wa kushindania mataji huku ukiandaa kizazi kijacho. Sasa Warriors wameamua kuwekeza akili yao yote kwenye miaka ya mwisho ya enzi ya Curry.
Kuachana na mustakabali
Kumtoa Kuminga ndiyo kiini cha kosa. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alikuwa daraja muhimu kati ya Warriors wa sasa na wa baadaye. Ana nguvu, uwezo wa kujilinda na bado alikuwa anakua kiuchezaji. Ingawa kulikuwa na mvutano kuhusu nafasi yake kikosini, thamani yake ya muda mrefu ilikuwa kubwa.
Kumtoa wakati thamani yake iko kwenye sintofahamu kunatikisa mambo kikosini. Badala ya kuwa mrithi wa Curry au sehemu ya dili kubwa zaidi siku zijazo, alibadilishwa kwa mchezaji mkubwa kwa umri na mwenye historia ya majeraha.
Hatari kubwa, uhakika mdogo
Kiusanii mpira wa kikapu, Porzingis anaendana vyema na mfumo wa kocha wa Golden State Warriors, Steve Kerr. Lakini, afya yake imekuwa kitendawili. Alifika akiwa bado anasumbuliwa na jeraha la mguu, na hakuna uhakika wa upatikanaji wake wakati wa mechi za 'play-in au play off'.
Kwa kufanya biashara hii, Warriors wamebadilisha uhakika wa kikosi kuwa na matumaini. Ikiwa Porzingis atarudi akiwa fiti uamuzi wao unaweza kuonekana wa kishujaa. Lakini kama atakumbwa tena na majeraha, dirisha la usajili la 2026 litakumbukwa kama wakati ambao Warriors walipoteza mwelekeo na labda, mustakabali wao.