KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Mzigo wote wa hatua ya makundi upo hivi Qatar

DOHA, QATAR. UFARANSA yupo Kylian Mbappe. Brazil ni fundi Neymar. Ureno ni ya Cristiano Ronaldo na Bernardo Silva. Argentina ya mkali Lionel Messi, Ujerumani yupo mwamba, Leroy Sane.

England yupo Harry Kane. Poland ni Robert Lewandowski, Senegal ni Sadio Mane. Ubelgiji ni Kevin De Bruyne na Uholanzi ni Frankie De Jong. Hayo ni majina machache makubwa yanayotazamiwa kuwapo kwenye viwanja vya kumsaka bingwa wa dunia.

Ni mchakamchaka wa fainali za Kombe la Dunia 2022. Mashabiki wa soka duniani wanasubiri kwa hamu kuanza kwa fainali hizo, Novemba 20 - kwa kawaida ya mikikimikiki ya Kombe la Dunia kila mbabe ana mbabe wake. Ukichapwa na huyu, nawe unatafuta mnyonge wa kumchapa. Ni vuta, nikuvute. Kila kitu kitajionyesha kwenye mechi za makundi.

Mzigo wa hatua ya makundi utaanzia kwa mwenyeji Qatar kukipiga na Ecuador, Novemba 20. Siku inayofuata, zitapigwa gemu tatu - England na Iran, Senegal na Uholanzi, wakati Marekani watakipiga na wageni wa fainali hizo, Wales ya Gareth Bale.

Siku ya tatu kutakuwa na mechi tatu - Argentina watachapana na Saudi Arabia, Denmark na Tunisia, Mexico na Poland na mabingwa Ufaransa watanyooshana na Australia. Siku ya nne kutakuwa na mechi nne - Morocco na Croatia ya Luka Modric, Ujerumani na Japan, Hispania na Costa Rica na Ubelgiji watamalizana na Canada kabla ya siku ya tano kushuhudia mechi nne za kukamilisha raundi ya mechi za kwanza, Uswisi watacheza na Cameroon, Uruguay na Korea Kusini, Ureno na Ghana na Brazil watakipiga na Serbia. Mechi za pili zitapigwa kati ya Novemba 25 hadi Novemba 28, ambapo siku ya kwanza, Wales wakicheza na Iran, Qatar na Senegal, Uholanzi na Ecuador na vita ya England na Marekani. Siku inayofuatia, Tunisia na Australia, Poland na Saudi Arabia, Ufaransa na Denmark na Argentina na Mexico.

Kisha zitafuata mechi za Japan na Costa Rica, Ubelgiji na Morocco, Croatia na Canada na Hispania wataonyeshana ubabe na Ujerumani. Siku ya mwisho za mechi za pili za makundi, Cameroon watacheza na Serbia, Korea Kusini na Ghana, Brazil na Uswisi na Ureno na Uruguay. Mechi za kukamilisha hatua ya makundi zitaanza Novemba 29 hadi Desemba 2.

Zitaanza kwa Ecuador kucheza na Senegal, Uholanzi na Qatar, Iran na Marekani na Wales na Waingereza wenzao, England. Siku inayofuata, Tunisia na Ufaransa, Australia na Denmark, Poland na Argentina na Saudi Arabia watakipiga na Mexico. Siku inayofuata Croatia watacheza na Ubelgiji, Canada na Morocco, Japan na Hispania na Costa Rica watamaliza ubishi na Ujerumani, huku siku ya mwisho ya hatua ya makundi itashuhudia, Korea Kusini wakicheza na Ureno, Ghana na Uruguay, Serbia na Uswisi na Cameroon na Brazil. Hivyo ndivyo utakavyokuwa mchakamchaka wa hatua ya makundi huko Qatar 2022.