Kombe la Dunia 2026 kuingiza faida ya Sh28.23 Trilioni
Muktasari:
- Mashindano hayo yatafanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za bara moja kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake mwaka 1930, hatua ambayo imeongeza mvuto wa kibiashara pamoja na kuongezeka kwa watazamaji duniani.
FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika kwa ushirikiano wa nchi za Marekani, Canada na Mexico, zinatarajiwa kuingiza mapato maradufu ya dola bilioni 10.9 (Sh28.23 Trilioni), na kuyafanya kuwa mashindano yenye faida kubwa zaidi katika historia.
Mashindano hayo yatafanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za bara moja kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake mwaka 1930, hatua ambayo imeongeza mvuto wa kibiashara pamoja na kuongezeka kwa watazamaji duniani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Sport Value, makadirio ya mapato hayo yanawakilisha ongezeko la asilimia 56 ukilinganisha na mashindano ya Kombe la Dunia 2022, ambayo yalipata takribani dola bilioni 7 (Sh18.12 Trilioni), na zaidi ya mara mbili ya dola bilioni 5.3 (Sh13.72 Trilioni) zilizopatikana mwaka 2018.
Ongezeko hili la mapato linaambatanishwa na upanuzi wa muundo wa mashindano, kuongezeka kwa watazamaji duniani, na mahitaji makubwa katika masoko ya kibiashara.
Hali ya mapato kwa sehemu:
Haki za matangazo ya televisheni zimedumishwa kama chanzo kikuu cha mapato, zikitarajiwa kufikia dola bilioni 4.2 (Sh10.87 Trilioni), ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Makubaliano ya udhamini yanakadiriwa kufikia kiwango cha juu zaidi, takriban dola bilioni 2.8 (Sh7.25 Trilioni), ongezeko la asilimia 59 ukilinganisha na mwaka 2022.
Mapato kutokana na tiketi na huduma za wageni yanatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa, takriban dola bilioni 3 (Sh7.76 Trilioni), kiasi sawa na mapato yote ya tiketi ya Mashindano sita ya mwisho ya Kombe la Dunia kwa pamoja.
Hii inatokana na kutarajia kujaa kwa viwanja vya michezo katika nchi tatu wenyeji pamoja na idadi kubwa ya mashabiki watakaosafiri kushuhudia mechi, ambapo mamilioni ya wapenzi wa soka wanatarajiwa kuhudhuria.
Wakati mashindano hayo yakikaribia, wachambuzi wanatabiri kwamba ongezeko hili la kifedha litathibitisha soka kama mchezo wenye mapato makubwa zaidi duniani na kuweka viwango vipya kwa matukio yajayo.
Kwa kuangaliwa kwa macho ya ulimwengu kote huko Amerika Kaskazini, Kombe la Dunia la 2026 linaonekana kuunganisha burudani ya michezo na mafanikio ya kibiashara, na kubadilisha matarajio ya kizazi kijacho kuhusu uzalishaji wa mapato katika soka.