Kocha mpya Liverpool ni nomaa

Muktasari:

  • Kwa wiki kadhaa sasa, Liverpool ilidaiwa kuweka kambi kwa kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim ikiamini atafaa kwenye kurithi kiti cha Klopp baada ya mpango wao wa kumchukua Xabi Alonso kukwama.

LIVERPOOL, ENGLAND: Ndo hivyo. Liverpool huenda ikapoteza fursa ya kumnasa kocha anayemtaka akachukue mikoba ya Jurgen Klopp huko Anfield baada ya kudaiwa kuingia kwenye mazungumzo ya kujiunga na timu nyingine ya Ligi Kuu England.

Kwa wiki kadhaa sasa, Liverpool ilidaiwa kuweka kambi kwa kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim ikiamini atafaa kwenye kurithi kiti cha Klopp baada ya mpango wao wa kumchukua Xabi Alonso kukwama.

Lakini, sasa Amorim ameripotiwa kuingia kwenye mazungumzo na klabu ya West Ham United, ambayo inafikiria kuachana na David Moyes mwishoni mwa msimu.

Awali kulikuwa na ripoti kwamba Amorim na mabosi wa Liverpool wamefanya makubaliano ya mdogo na Mreno huyo atasaini mkataba wa miaka mitatu huko Anfield itakapofika mwisho wa msimu huu ambapo Klopp atang'atuka na kwenda mapumziko.

Amorim, 39, ameiweka patamu Sporting ikiongoza kwa tofauti ya pointi saba huko kwenye msimamo wa Primeira Liga na mwezi ujao timu yake itacheza na FC Porto kwenye fainali ya Taca de Portugal.

Kuna nyakati pia alihusishwa na miamba ya Hispania, Barcelona ambao wataachana na kocha wao Xavi mwishoni mwa msimu. Kinachoelezwa ni kuvunja mkataba wa Amorim huko Sporting, inahitajika Pauni 12.9 milioni.

Kuibuka kwa Barcelona na sasa West Ham wanaomtaka kocha Amorim, jambo hilo linawaweka Liverpool kwenye shida kubwa katika kutambua mapema ni kocha gani atakayekuja kuchukua mikoba ya Klopp atakoondoka mwisho wa msimu.

Siku za karibuni ilidaiwa kwamba Liverpool inaweza kumfikiria kocha wa Brighton, Roberto De Zerbi, lakini pia kuna mpango wa kumjaribu Jose Mourinho kama atakuwa tayari kwenda kufanya kazi Anfield, huku kocha mwingine kwenye rada ya wakali hao wa Merseyside ni Ange Postecoglou wa Tottenham Hotspur.