Kocha Liverpool agomea tuzo
Muktasari:
- Tuzo hizo ambazo zilitolewa saa chache baada ya kichapo hicho, Slot alikuwa akiwania ya Kocha Bora wa Mwaka, lakini alikataa kuhudhuria na hivyo kulazimika kutumwa mwakilishi wa kuchukua tuzo hizo.
LIVERPOOL, ENGLAND: KIPIGO cha mabao 3-0 ilichopata Liverpool kutoka kwa Nottingham Forest mechi ya Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita, kimemvuruga kocha wa majogoo hao, Andre Slot na kuzisusia tuzo zilizokuwa zikitolewa na Chama cha waandishi wa Habari za Northern Football Writers’ Association.
Tuzo hizo ambazo zilitolewa saa chache baada ya kichapo hicho, Slot alikuwa akiwania ya Kocha Bora wa Mwaka, lakini alikataa kuhudhuria na hivyo kulazimika kutumwa mwakilishi wa kuchukua tuzo hizo.
Slot alishinda tuzo hiyo baada ya kuiongoza Liverpool kutwaa taji la Ligi Kuu England ukiwa ni msimu wake wa kwanza, ingawa miezi michache baadaye katika kuijenga timu amejikuta katika wakati mgumu kutokana na kusuasua na amepoteza mechi nane kati ya 11 zilizopita za michuano yote.
Hata hivyo, Liverpool ililazimika kumtuma balozi wa klabu, Gary McAllister aliyekuwa akienda kuhudhuria mechi kati ya Leeds dhidi ya Aston Villa, kumwakilisha kocha huyo, 47 aliyethibitisha hatakuwepo kwenye hafla ya Jumapili jioni.
Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo kwa niaba ya Slot, McAllister alitoa ujumbe mfupi kutoka kwa kocha huyo Mholanzi uliosema “anajivunia sana” kushinda tuzo hiyo.
Katika tuzo hizo makocha wengine waliotunukiwa ni Daniel Farke wa Leeds, Phil Parkinson wa Wrexham na Eddie Howe wa Newcastle.
Meneja wa mwisho kutoka Ligi Kuu England aliyeshinda tuzo hiyo ni Erik ten Hag, aliyoyepewa mwaka jana baada ya kuipa Manchester United Kombe la la FA msimu wa 2023–24, hata hivyo, siku chache baadaye kocha huyo Mholanzi alitimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Ruben Amorim.
Kichapo hicho kutoka kwa Forest ambao wamepata ushindi wa pili mfululizo katika Uwanja wa Anfield kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978, kilimvuruga Slot na baada ya mechi hiyo amesema lawama zote anastahili yeye;
“Nataka kusisitiza mimi ndiye niliye na jukumu la matokeo haya mabaya. Unawajibika unaposhinda, pia unapopoteza. Siwezi kutoa visingizio vya kutosha kwa matokeo haya. Hayatoshi kabisa na mimi ninawajibika.”