I'm sorry, Slot akubali lawama Liverpool
Muktasari:
- Jana Jumamosi, Nottingham Forest ilipata ushindi mkubwa zaidi chini ya Kocha wao mpya, Sean Dyche kuichapa Majogoo hao mabao 3-0 kwa mabao ya Mabao ya Murillo, Nicolo Savona na Morgan Gibbs-White.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amesema anapaswa kubeba lawama kutokana na matokeo mabaya mfululizo ya timu yake tangu mwanzo wa msimu huu.
Jana Jumamosi, Nottingham Forest ilipata ushindi mkubwa zaidi chini ya Kocha wao mpya, Sean Dyche kuichapa Majogoo hao mabao 3-0 kwa mabao ya Mabao ya Murillo, Nicolo Savona na Morgan Gibbs-White.
Kichapo hicho kiliongeza machungu kwa Liverpool, hii ikiwa ni mechi ya nane kwao kupoteza kati ya 11 za michuano yote msimu huu na sasa imetupwa hadi nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Akizungumza baada ya mechi, Slot amesema: "Mimi ndiye ninayepaswa kuwajibika kwa vipigo hivi tunavyopata. Unaposhinda unawajibika na unapopoteza pia unawajibika. Siwezi kutoa visingizio kwa matokeo tunayopata. Ni jukumu langu kuwajibika pale timu inaposhinda au kupoteza."
"Kikubwa ninachokiona katika timu bado kuna ushirikiano, mashabiki wetu walibaki hadi mwisho wa mchezo licha ya kuongozwa kwa muda mwingi, haikuwa hivyo dhidi ya Manchester City (wiki mbili zilizopita)," amesema Slot na kuongeza katika mechi ya Forest aliona utofauti mkubwa kwa wachezaji wake na walau walitengeneza nafasi nyingi.
"Hivi karibuni, mara kwa mara, tumekuwa tukikosa nafasi za kufunga mabao kisha tunaruhusu sisi, hilo haliwezi kuendelea msimu mzima, tunahitaji kufunga mabao, ukiwa unatawala mechi na kufunga bao moja mpinzani hupoteza morali. Lakini kilichotokea katika mechi hii ni kinyume na wao walipata morali kubwa baada ya kufunga bao la kwanza."
Alipoulizwa juu ya utata wa bao la kwanza la Forest, Slot bado aliendelea kusisitiza hakuna kisingizio chochote kwa sasa badala yake yeye ndiye anatakiwa alaumiwe.
Liverpool itakuwa mwenyeji wa PSV ya Uholanzi kesho Jumatano katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na baada ya hapo itakutana na West Ham Jumapili ya wikiendi ijayo kabla ya kuwa na kibarua kigumu dhidi ya Sunderland.