Kisa Florian Wirtz, Wajerumani wamshutumu Mo Salah
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na Sport Bild na kunukuliwa na Liverpool.com, Salah anatuhumiwa kushindwa kuwaunganisha wachezaji wapya, hususan Wirtz, ambaye amekuwa chini ya kiwango tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Bayer Leverkusen kwa dau la takribani Euro 140 milioni.
Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, ametupiwa lawama na baadhi ya vyombo vya habari vya Ujerumani, vikidai anahusika na mwanzo mgumu wa Florian Wirtz katika klabu hiyo ya Anfiled.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na Sport Bild na kunukuliwa na Liverpool.com, Salah anatuhumiwa kushindwa kuwaunganisha wachezaji wapya, hususan Wirtz, ambaye amekuwa chini ya kiwango tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Bayer Leverkusen kwa dau la takribani Euro 140 milioni.
Wirtz, mwenye umri wa miaka 23, bado hajafunga bao, lakini ametoa pasi tatu za mabao katika mechi 16 alizocheza hadi sasa, huku akiwa hajatoa mchango wa pasi ya mabao katika Ligi Kuu ya England. Licha ya kung’ara katika mechi za kimataifa, nafasi yake ndani ya kikosi cha Kocha Arne Slot bado imeibua mjadala.
Sport Bild imeandika kuwa, Salah amekuwa akimpotezea Wirtz wanapokuwa uwanjani na amekuwa akionyesha kutowasaidia wachezaji wapya kwa kiwango kinachotarajiwa.
Ripoti hiyo imesema: “Ni dhahiri kuwa amekuwa akimpuuza Wirtz na hajawawezesha wachezaji wengine wapya, ambao thamani yao kwa pamoja inakaribia euro nusu bilioni. Salah anazidi kuwa tatizo kwa Liverpool na kwa Wirtz.”
Wachambuzi hao waliongeza kuwa, Salah, ambaye ametoa pasi tatu za mabao msimu huu kwa wachezaji waliokuwapo klabuni kwa muda mrefu, anaonekana kuzuia maendeleo ya vizazi vipya vya safu ya ushambuliaji ya Liverpool.
Aidha, uchambuzi huo umetaja uwezekano wa winga huyo wa Misri kuhamia Saudi Arabia mwaka 2026, ukidai kwamba klabu, kocha, au wachezaji wenzake huenda wakalazimika kumshinikiza aoondoke ili kutoa nafasi kwa Wirtz kuongoza mashambulizi ya timu kwa siku zijazo.