Kocha Chelsea awakingia kifua mastaa
Muktasari:
- Ndani ya kipindi cha siku 10 Chelsea imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain, ikapoteza nyumbani dhidi ya Newcastle United na kisha ikachapwa vibaya na Everton wikiendi iliyopita hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya kumaliza katika nafasi tano za juu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Liam Rosenior amekanusha vikali madai kwamba wachezaji wa klabu hiyo hawajitoi vya kutosha baada ya kipigo cha mabao 3-0 ugenini dhidi ya Everton.
Ndani ya kipindi cha siku 10 Chelsea imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain, ikapoteza nyumbani dhidi ya Newcastle United na kisha ikachapwa vibaya na Everton wikiendi iliyopita hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya kumaliza katika nafasi tano za juu.
Katika kipindi hicho ambacho Chelsea imepoteza mechi nne kwa jumla ya mabao 12 kulikuwa pia na kauli kutoka kwa Enzo Fernandez zilizofichua kuwa mastaa hawakupenda kuondoka kwa Enzo Maresca hali iliyosababisha timu kubadilika kimuundo na kimfumo.
“Kwa upande wangu sidhani kama kuna ukosefu wa wachezaji kujitoa. Mfano Enzo Fernandez ulimuona aliendelea kupambana hadi dakika ya mwisho leo. Ninaelewa unapokuwa kwenye mfululizo wa vipigo kama ilivyo sasa na unapokuwa na kiwango cha uchezaji kama tulichokuwa nacho mambo hayo huanza kusemwa. Lakini sidhani kama hilo ndilo tatizo kwa sasa.”
Mashabiki wenye hasira walionyesha hisia zao kwa Rosenior baada ya mechi ambapo wengi wao waliondoka kabla ya filimbi ya mwisho na kocha huyo alikiri kuwa anaumizwa na matokeo wanayoyapata kama wao wanavyoumia. “Najua wanalipia kuja uwanjani wanaipenda klabu hii na wamekuja kutoka mbali. Hiki ni kipindi kigumu kwa klabu. Mimi ni kazi yangu lakini naumia pia. Bila kujali nafasi yako kwenye ligi inauma kupoteza mechi yoyote ile. Inabidi tushikamane. Tuko nyuma kwa pointi moja tu kufikia nafasi ya Ligi ya Mabingwa. Tunapaswa kuendelea kuwapa wachezaji hali ya kujiamini kadri inavyowezekana.”