Kocha Chelsea ataka beki mwingine
Muktasari:
- Maresca alisema The Blues inahitaji beki mwingine kwa sababu waliopo kwenye timu hiyo kwa sasa hawana uwezo wa kuziba pengo la Mwingereza huyo.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amesema timu hiyo inahitaji kusajili beki mpya wa kati baada ya kumpoteza Levi Colwill kwa majeraha makubwa ya goti.
Maresca alisema The Blues inahitaji beki mwingine kwa sababu waliopo kwenye timu hiyo kwa sasa hawana uwezo wa kuziba pengo la Mwingereza huyo.
Akizungumza kabla ya mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace, Maresca alisema: “Levi anafahamu kwamba atakuwa nje kwa muda mrefu. Hili ni pigo kubwa kwetu. Unajua jinsi Levi alivyokuwa muhimu kwetu msimu uliopita, hasa kwa mtindo wetu tunaotaka kucheza.
“Tulisema mara nyingi tunaweza kutengeneza nafasi za kushambulia kwenye upande wa kulia kutokana na namna tulivyotengeneza eneo hilo. Levi amekuwa sehemu muhimu wa kujenga mashambulizi yetu na sasa atakuwa nje ya uwanja, hivyo tutahitaji kuwa na suluhisho tofauti. Tunajaribu kutafuta suluhisho, lakini klabu inafahamu kitu gani ninachofikiria.”€
Maresca aliongeza: “Nadhani tunahitaji kuongeza beki wa kati. Tumejaribu kuangalia suluhu kutokea ndani, lakini kama nilivyosema, klabu inafahamu wazi kitu ninachofikiria.”€
Maresca alisema hakuna beki yeyote kati ya Tosin Abarabioyo, Wesley Fofana na Benoit Badiashile mwenye uwezo wa kucheza kama Levi kulingana na mipango yao ndani ya uwanja na ndiyo maana anafikiria kuingia sokoni kunasa beki mpya.