Kobbie Mainoo ndo hivyo tena

Muktasari:

  • Mainoo, 18, amekuwa mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha Man United kwa sasa chini ya Kocha Erik ten Hag.

MANCHESTER, ENGLAND: Manchester United imepanga kumpa ofa ya dili safi kabisa kiungo Kobbie Mainoo huku bilionea mpya wa miamba hiyo ya Old Trafford, Sir Jim Ratcliffe akitaka kujenga kikosi kipya kutokana na kinda huyo.


Mainoo, 18, amekuwa mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha Man United kwa sasa chini ya Kocha Erik ten Hag.


Man United inataka kumwongezea mshahara Mainoo kwa sababu inamhesabu kama mmoja wa wachezaji ambao wapo kwenye mipango mipya ya bilionea Ratcliffe katika kuifumua na kuifuma upya timu hiyo ili kuwa tishio uwanjani.


Fabrizio Romano alisema: “Ipo hivi, Manchester United kwa sasa ipo kwenye mazungumzo ya kumwongezea mkataba Kobbie Mainoo itakapofika mwisho wa msimu na mjadala huo ulianza Februari.


“INEOS (Kampuni ya bilionea Ratcliffe) inamtaka Kobbie awe mmoja wa mastaa wataokuwa kwenye mpango mpya wa timu hiyo. Dili jipya litashuhudia mshahara wa Mainoo ukiongezeka pamoja na bonasi kadhaa.” Kiungo huyo anaripotiwa kulipwa Pauni 20,000 kwa wiki na sasa kuna kila dalili mshahara wake ukaongezeka mara tatu atakaposaini dili jipya la kubaki Old Trafford.

Mainoo amecheza mechi 27 kwenye kikosi cha Man Unied kwenye michuano yote msimu huu na amefunga mabao matatu na asisti mbili. Amejumuishwa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England, wakati kikosi hicho cha Kocha Gareth Southgate kilipocheza na Brazil na Ubelgiji kwenye mechi za kirafiki.


Mainoo amekuwa kwenye kikosi cha Man United tangu alipokuwa na umri wa miaka tisa. Makinda wengine wanaotazamiwa kuwapo kwenye mpango mpya wa Man United ni Alejandro Garnacho na beki wa kati Willy Kambwala.