Kobbie Mainoo anukia Newcastle United
Muktasari:
- Mainoo ameanza mara moja kwenye mechi za Ligi Kuu England msimu huu, na kocha Amorim ameweka wazi kwamba hamtumii kwa sababu bado hajafikia katika hali ambayo anahitaji awe nayo.
NEWCASTLE United inapanga kuwasilisha ofa katika dirisha lijalo la majira ya baridi mwakani ili kumsajili kiungo wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Kobbie Mainoo, 20, ikiwa ataendelea kupata nafasi ndogo ya kucheza chini ya kocha Ruben Amorim.
Mainoo ameanza mara moja kwenye mechi za Ligi Kuu England msimu huu, na kocha Amorim ameweka wazi kwamba hamtumii kwa sababu bado hajafikia katika hali ambayo anahitaji awe nayo.
Newcastle United inaamini kwamba anaweza kuimarisha eneo la kiungo ambalo mara kadhaa limekuwa likikumbana na changamoto ya majeraha ya mastaa tegemeo wakiwamo Sandro Tonali na Bruno Guimaraes.
Mkataba wa sasa wa Mainoo unatarajiwa kumalizika ifikapo 2027 na msimu uliopita alicheza mechi 37 akafunga mabao mawili. Katika dirisha lililopita Mainoo alihitaji sana kuondoka, lakini Man United iligoma kumuuza na kusisitiza kwamba bado anahitajika kwenye timu.
William Saliba
REAL Madrid na Paris Saint-Germain zimeendelea kumfuatilia beki kisiki wa Arsenal na timu ya taifa Ufaransa, William Saliba ambaye Washika Mitutu wanaendelea kufanya naye mazungumzo ya mkataba mpya ili wamuongezee. Supastaa huyo ambaye mkataba wake unamalizika 2027, amekuwa akiwindwa na Real Madrid tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Adam Wharton
CHELSEA imeongeza juhudi katika mchakato wa kumnunua kiungo wa Crystal Palace na England, Adam Wharton kwenye dirisha lijalo la majira ya baridi. Mabosi wa Palace wanadaiwa kuhitaji kati ya Pauni 55 hadi 60 milioni ilikumuuza staa huyo ambaye walikataa kumuuza dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa sababu kocha alihitaji huduma yake kufanikisha malengo ya msimu huu.
James Garner
EVERTON inataka kuingia sokoni wiki chache zijazo dirisha la usajili la Januari ili kusajili beki wa pembeni kwa usajili huru iwapo majeraha ya James Garner na Nathan Patterson yataendelea. Kwa sasa inafuatilia wachezaji huru waliowahi kucheza EPL na La Liga ikiamini hawatahitaji muda mwingi kuingia katika mifumo. Miongoni mwao ni Ryan Bertrand.
Sergio Reguilon
WEST Ham United, Everton na Nottingham Forest zinafikiria kumsajili beki wa kushoto wa zamani wa Tottenham Hotspur, Sergio Reguilon, 28, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuachana na Spurs dirisha lililopita la kiangazi. Mbali ya England, Reguilon pia anawindwa na timu za Serie A na La Liga. Everton inaweza kumchukua kusaidia suluhisho la majeraha.
Ronald Araujo
MABOSI wa Liverpool wanamfuatilia beki wa Barcelona, Ronald Araujo ili akawe mbadala wa Ibrahima Konate ambaye amekataa kusaini mkataba mpya na kuna uwezekano akaondoka bure mwisho wa msimu kujiunga na Real Madrid. Barcelona ipo tayari kumuuza, lakini kwa dau lisilopungua Euro 70 milioni. Araujo amesisitiza mara kadhaa kwamba anafurahia kuwapo Barcelona.
Nicolas Jackson
WAKALA wa staa wa Chelsea, Nicolas Jackson ameweka wazi kuwa staa huyo hataki kurejea Chelsea msimu ujao baada ya mkataba wa mkopo na Bayern Munich kumalizika mwisho wa msimu. Jackson alikataa kurudi Chelsea dirisha lililopita baada ya mabosi wa timu hiyo kuiambia Bayern kwamba haitaki kumtoa kwa mkopo.
Ayyoub Bouaddi
LIVERPOOL ipo katika nafasi nzuri ya kumsajili kiungo wa Lille na Ufaransa, Ayyoub Bouaddi mwenye umri wa miaka 17. Hadi sasa taarifa za awali zinaeleza kwamba timu zote zinapambana kuhakikisha kwamba zinamsa, lakini hakuna hata timu moja iliyowasilisha ofa ya kumsajili. Bouaddi amevutia vigogo wengi kutokana na kipaji kikubwa alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu.