Kisa Liverpool, Enzo Maresca arusha taulo mapema
Muktasari:
- Liverpool ambayo imecheza mechi tano za EPL kwa sasa inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 15 ikiwa ni tofauti ya alama tano dhidi ya timu iliyopo nafasi ya pili.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amesema kiwango ambacho Liverpool imekionyesha katika mechi tano za mwanzo za msimu huu kinaonyesha kuwa ni ngumu kuwafikia wapinzani wao hao na wana nafasi kubwa ya kushinda taji la Ligi Kuu England.
Liverpool ambayo imecheza mechi tano za EPL kwa sasa inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 15 ikiwa ni tofauti ya alama tano dhidi ya timu iliyopo nafasi ya pili.
Ushindi wa Liverpool katika dabi ya Merseyside uliendeleza mwanzo mzuri katika kutetea taji kwani imebaki kuwa timu pekee ambayo haijapoteza hata mechi moja Ligi Kuu England msimu huu.
Liverpool ilipata faida ya kuongoza kwa pointi nyingi baada ya kuichapa Arsenal ambayo ndio mpinzani wake wa karibu katika msimamo.
Hadi sasa mabingwa hao watetezi wana tofauti ya pointi tano mbele ya Arsenal, saba mbele ya Chelsea na nane mbele ya Man City.
Kiwango ambacho kimeonyeshwa na Majogoo hao kinaonekana kumvunja nguvu Maresca ambaye anaamini itakuwa kazi kubwa kushindana nao msimu huu ikiwa wataendelea kupata matokeo mazuri.
“Iwapo wataendelea hivi ninaona haitawezekana kuwafikia. Siyo kwetu tu, bali kwa klabu nyingine zote. Wamefanya kazi kubwa tangu mwaka jana na wachezaji waliokuwa wanawanunua wanaonyesha uchu na kiu ya kuhakikisha klabu inafanya vizuri zaidi, hilo liko wazi kabisa.”
Mwanzo mzuri wa Liverpool msimu huu umeendelea pia katika mashindano ya Ulaya ambapo iliibuka na ushindi katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid kwenye Uwanja wa Anfield katika mchezo ambao ilishinda dakika za jioni kwa bao la Virgil van Dijk.
Liverpool inapambana kushinda mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.
Usajili wa wachezaji wapya unaonekana kuongeza upya nguvu katika kikosi hicho na ari ya kupambana zaidi jambo linaloifanya timu hiyo kuwa tishio.
Katika dirisha lililopita la usajili Liverpool ilitumia takribani Pauni 400 milioni kusajili wachezaji wapya ambapo ilivunja rekodi ya usajili ya England kwa kuwachukua Florian Wirtz kutoka Bayer Leverkusen na baadaye Alexander Isak aliyetoka Newcastle United.
Arsenal ilitabiriwa kuwa mpinzani wa karibu waLiverpool, lakini haionekani kufanya hivyo na tayari imeanza msimu ikiwa na changamoto ya majeraha kwa wachezaji wake tegemeo akiwemo Noni Madueke ambaye atakuwa nje kwa kipindi kisichopungua miezi miwili.