Kipa Courtois ajitosa kwenye kumiliki timu
Muktasari:
- Nyota huyo wa Ubelgiji amekuwa mmiliki mwenza wa Le Mans FC ya Ufaransa, akijiunga na kundi la wawekezaji linalomjumuisha gwiji wa tenisi Novak Djokovic pamoja na mastaa wa Formula One, Felipe Massa na Kevin Magnussen.
MADRID, HISPANIA: KIPA wa Real Madrid, Thibaut Courtois, ndiye mwanasoka wa hivi karibuni aliyejiunga kwenye orodha ya wamiliki wa klabu za soka.
Nyota huyo wa Ubelgiji amekuwa mmiliki mwenza wa Le Mans FC ya Ufaransa, akijiunga na kundi la wawekezaji linalomjumuisha gwiji wa tenisi Novak Djokovic pamoja na mastaa wa Formula One, Felipe Massa na Kevin Magnussen.
Courtois, mwenye umri wa miaka 33, amenunua hisa kupitia kampuni ya uwekezaji ya NxtPlay, ambayo aliianzisha kwa ushirikiano na wengine.
Ilianzishwa mwaka 1985, klabu hiyo ya Ufaransa kwa sasa inashiriki Ligue 2, baada ya kuwahi kucheza Ligue 1 kati ya mwaka 2005 hadi 2010. Kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, lakini iko pointi tatu tu nyuma ya kinara, ES Troyes AC.
Klabu hiyo imepewa jina la utani la “Wrexham ya Ufaransa” kutokana na uwekezaji wa watu mashuhuri na kupanda kwao kwa kasi kutoka madaraja ya chini.
Le Mans ilitangaza rasmi mwezi Agosti mwaka jana, kampuni ya uwekezaji ya OutField ilinunua asilimia fulani ya klabu ambayo haikuwekwa wazi.
Katika taarifa iliyochapishwa na Le Mans, walieleza Djokovic, mshindi mara 24 wa mashindano ya Grand Slam, ataleta mchango chanya kwa klabu hiyo. Taarifa hiyo ilisema: “Uimara wake wa kiakili na mtazamo wake wa kipekee vitaleta thamani kubwa sana.”
Kuhusu Massa na Magnussen, klabu ilisema wawili hao wataunda daraja kati ya soka na michezo ya magari jambo ambalo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Le Mans.
Miaka tisa iliyopita, Le Mans ilikuwa ikicheza soka la kiwango cha chini daraja la tano baada ya kukumbwa na matatizo ya kifedha, sawa na yaliyowahi kuikumba RC Strasbourg Alsace.
Lakini sasa kwa uwekezaji wa Courtois, ambaye pia ni nyota wa zamani wa Chelsea, ndoto yao ya kushindana Ligue 1 iko karibu kuwa kweli.
Le Mans hucheza mechi zao za nyumbani katika Uwanja wa Stade Marie-Marvingt, uliopo karibu na uwanja maarufu wa mashindano ya magari.
Uwekezaji katika klabu vya soka unazidi kuwa jambo la kawaida miongoni mwa wanasoka wa sasa na wa zamani, mifano maarufu ni pamoja na David Beckham, mmiliki mwenza wa Inter Miami; Kylian Mbappe, mmiliki mkuu wa SM Caen; Luka Modric, aliyejiunga na kundi la wamiliki wa Swansea City, Aprili 2025.
Wachezaji wengine wa zamani wa Chelsea pia wamehusika katika umiliki wa klabu, wakiwemo Eden Hazard na Demba Ba (San Diego FC), Didier Drogba (Phoenix Rising FC) na N'Golo Kante (Royal Excelsior Virton).