Kipa amtwisha ngumi beki Hispania
Muktasari:
- Kabla ya tukio hilo, Andrada alikuwa tayari ameonyeshwa kadi nyekundu baada ya kupata kadi ya pili ya njano kufuatia kumsukuma Pulido.
ZARAGOZA, HISPANIA: KIPA wa Real Zaragoza, Esteban Andrada yuko kwenye hatari ya kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu baada ya kumpiga ngumi beki wa timu pinzani wakati wa mechi ya ligi daraja la pili nchini Hispania.
Tukio hilo lilitokea wakati wa dabi dhidi ya Huesca na Andrada alimshambulia Jorge Pulido kwa ngumi ya uso, tukio lililosababisha vurugu kubwa uwanjani.
Kabla ya tukio hilo, Andrada alikuwa tayari ameonyeshwa kadi nyekundu baada ya kupata kadi ya pili ya njano kufuatia kumsukuma Pulido.
Baada ya Pulido kusimama, Andrada alimkimbilia na kumpiga ngumi kali usoni, hatua iliyozua ugomvi mkubwa uliowahusisha wachezaji na mabenchi ya timu zote mbili.
Katika vurugu hizo, hata kipa wa Huesca, Dani Jimenez, alijaribu kulipiza kisasi kwa kumpiga Andrada nyuma ya kichwa.
Baada ya tukio hilo katika mchezo huo ambao Huesca iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Andrada aliomba radhi akisema alipoteza umakini na kujikuta akifanya kitendo kisichofaa.
Amesema: “Ninaomba radhi sana kwa kilichotokea. Siyo picha nzuri kwa klabu wala kwa mashabiki. Nilipoteza ustamihilivu wangu kwa muda mfupi.”
Kocha wa Huesca, Jose Luis alikosoa tukio hilo akisema halikubaliki licha ya presha ya mchezo huo.