Kimmich, wenzake kulipia mashabiki nauli Kombe la Dunia
Muktasari:
- Nyota hao wamefikia hatua hiyo baada mashabiki wengi wakilalamikia kupanda kwa bei za usafiri kuelekea viwanjani, hususani katika eneo la New York na New Jersey ambako Ujerumani itacheza dhidi ya Ecuador Juni 25 kwenye Uwanja wa MetLife.
WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Ujerumani wameamua kugharamia usafiri wa mashabiki 600 katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi E wa Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka malalamiko kuhusu gharama za usafiri katika mashindano hayo huko Marekani, Canada na Mexico.
Nyota hao wamefikia hatua hiyo baada mashabiki wengi wakilalamikia kupanda kwa bei za usafiri kuelekea viwanjani, hususani katika eneo la New York na New Jersey ambako Ujerumani itacheza dhidi ya Ecuador Juni 25 kwenye Uwanja wa MetLife.
Awali tiketi za treni kutoka katikati ya jiji la New York kwenda uwanjani hapo zilikuwa zikigharimu dola 12.90 (zaidi ya Sh33,000), lakini bei hizo zilipandishwa hadi dola 150 (zaidi ya Sh385,000) kabla ya kushushwa hadi dola 98 (zaidi ya Sh251,000) kufuatia presha kutoka kwa mashabiki.
Mbali na treni, nauli za mabasi maalumu yaliyopangwa kuwapeleka mashabiki viwanjani zilianza kwa dola 80 (zaidi ya Sh205,000) kwa safari hiyohiyo kabla ya kupunguzwa hadi dola 20 (zaidi ya Sh51,000) baada ya malalamiko kuongezeka.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB), nahodha wa timu hiyo, Joshua Kimmich, pamoja na wachezaji wenzake wameamua kulipia mabasi yatakayowasafirisha mashabiki hao bila malipo kwenda kushuhudia mechi dhidi ya Ecuador.
DFB ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kama ishara ya kuthamini sapoti kubwa ambayo timu hiyo imekuwa ikipata kutoka kwa mashabiki wake katika mashindano hayo.
"Tukizingatia gharama kubwa za usafiri wa mabasi na treni katika eneo la New York wakati wa Kombe la Dunia, wachezaji wa timu ya taifa wameandaa usafiri wa bure kwa mashabiki 600 kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi," ilisema taarifa ya DFB.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Kimmich na wenzake ndio watakaobeba gharama zote za mabasi hayo yatakayowasafirisha mashabiki kutoka New York kwenda New Jersey kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
Suala la gharama za usafiri limeendelea kuzua mjadala katika Kombe la Dunia 2026 huku mashabiki kutoka mataifa mbalimbali wakieleza kuwa wanalazimika kutumia fedha nyingi zaidi kuliko walivyotarajia ili kufika viwanjani.
Katika fainali mbili zilizopita zilizofanyika nchini Russia mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022, mashabiki walikuwa wakipatiwa huduma za usafiri bure kwenda kwenye viwanja vya mechi na maeneo maalumu ya mashabiki.
Marekani ambao ni miongoni mwa wenyeji wa mashindano ya mwaka huu, waliahidi kutoa huduma kama hiyo katika makubaliano yake ya awali ya kuandaa Kombe la Dunia yaliyofikiwa mwaka 2018.
Hata hivyo, marekebisho yaliyofanywa mwaka 2023 yalibadili utaratibu huo na kuamua kwamba mashabiki watatozwa gharama za usafiri kulingana na thamani halisi ya huduma hizo, jambo ambalo limekuwa chanzo cha malalamiko hayo.