Kilio champa ujiko Thiago Silva

Muktasari:

  • Katika mchezo ambao Man City ilishinda 1-0 lililofungwa Bernardo Silva katika dakika za nyongeza, alionekana akimwaga machozi wakati yupo katika benchi la matajiri hao wa Jiji la London muda mfupi baada ya mechi kumalizika.

LONDON, ENGLAND. BEKI mkongwe wa Chelsea, Thiago Silva ambaye ameripotiwa kuwa ataondoka mwisho wa msimu amesifiwa na mashabiki baada ya kuonekana akilia uwanjani kwa timu yake kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City uliopigwa wikiendi iliyopita kwenye dimba la Wembley.

Katika mchezo ambao Man City ilishinda 1-0 lililofungwa Bernardo Silva katika dakika za nyongeza, alionekana akimwaga machozi wakati yupo katika benchi la matajiri hao wa Jiji la London muda mfupi baada ya mechi kumalizika.

Wakati Thiago akilia, staa mwingine wa Chelsea, Noni Madueke alionekana akicheka alipokuwa anaongea na winga wa Man City, Jack Grealish.

Mashabiki wengi walioona video hiyo kupitia mitandao mbalimbali walimsifia Silva kwa kusema kama wangekuwa na wachezaji watatu au wanne kama yeye basi muda huu Chelsea ingekuwa imeshashida taji lolote ama ingekuwa katika nafasi nzuri ya kushinda.

Mashabiki wengine waliandika maoni na kutaka Silva asainishwe mkataba mpya na asiondoke mwisho wa msimu kama inavyoelezwa.

Mkataba wa sasa wa Silva unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote juu ya kumuongeza ikiwa ni ishara kwamba anaondoka.

Staa huyu wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 39, alijiunga na Chelsea mwaka 2020 akitokea Paris Saint-Germain na katika misimu minne aliyodumu katika kikosi hicho hadi sasa ameonyesha kiwango bora na kuwa mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza licha ya umri kumtupa mkono akifukuzia kuingia miaka 40 mwakani.