Kesi ya matumizi... Manchester City kufanywa mfano England
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanakaribia kwenye siku ya hukumu baada ya kesi hiyo kujadiliwa kwa muda mrefu na Kocha Pep Guardiola mapema mwezi huu alisema mwezi ujao kila kitu kitafahamika.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City huenda ikakumbana na balaa la kushushwa daraja endapo itakutwa na hatia ya kuzidisha matumizi kwenye kesi ya kukiuka kanuni za mapato na matumizi katika usajili.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanakaribia kwenye siku ya hukumu baada ya kesi hiyo kujadiliwa kwa muda mrefu na Kocha Pep Guardiola mapema mwezi huu alisema mwezi ujao kila kitu kitafahamika.
Alipozungumza Februari 7, Guardiola alisema: “Ndani ya mwezi, nadhani hukumu itatoka.”
Kinachoelezwa, Man City itafanywa mfano endapo itakutwa na hatia ili kuzionyesha timu nyingine kinachoweza kuwakuta zikikiuka ishu ya usawa kwenye mapato na matumizi. Lakini, adhabu hiyo haitakuwa ya kuwazuia wasiingie kwenye mashindano ya EFL - ambayo yanaweza kuwa kwenye Championship, League One au League Two - inategegemea na kanuni za ligi husika.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya pesa kwenye timu za soka, Kieran Maguire - akizungumzia kesi hiyo ya Man City, alisema kitu kinachoweza kutokea ni kupokwa pointi, lakini kwa hali ilivyo kwenye timu hiyo, wanaweza kupokwa pointi mara sita ya adhabu iliyowahi kuwakuta Everton ilipokiuka ishu ya matumizi.
“Kupokwa pointi ni adhabu inayotazamwa kwa uharaka endapo itakutwa na hatia,” alisema Maguire.
“Ukubwa wa pointi zinazopunguza zinatofautiana, kama Everton ilipewa adhabu ya kupokwa pointi 10 na kwa sababu tu ilizidisha kati ya Pauni 10 milioni au Pauni 12 milioni kwa msimu mmoja. Nadhani ili kuweka mfano mzuri kwenye soka, adhabu hii itakuwa kali zaidi.”
Kinachoelezwa Man City inaweza kupunguzwa pointi kati ya 60 hadi 100, ambazo zinawasukuma kabisa kwenye kushuka daraja kwenye Ligi Kuu England na kwenda kucheza ligi za chini ambazo zipo chini ya EFL.