Keane: Pep Guardiola acha kujitetea
Muktasari:
- Kauli hiyo, ikamwibua mchambuzi na nyota wa zamani wa Manchester United, Roy Keane na kuielezea ‘siyo hoja ya msingi’ na Pep hana cha kujitetea kutokana na matokeo anayoyapata.
MANCHESTER, ENGLAND: JUZI Jumapili usiku, Machester City ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England, huku Kocha Pep Guardiola akijitetea ratiba na uchovu vimesababisha matokeo yasiyoridhisha ya timu yake.
Kauli hiyo, ikamwibua mchambuzi na nyota wa zamani wa Manchester United, Roy Keane na kuielezea ‘siyo hoja ya msingi’ na Pep hana cha kujitetea kutokana na matokeo anayoyapata.
Bao la kusawazisha la dakika ya 90+3 la Gabriel Martinelli kwenye Uwanja wa Emirates, liliinyima City ushindi wa pointi tatu baada ya kutangulia kufunga dakika ya 9, Erling Haaland akiweka kambani bao lake la sita la msimu huu Ligi Kuu England.
“Kama unazungumzia uchovu na ratiba, tuko mwezi wa Septemba na ilitoka kucheza mechi mbili nyumbani, dhidi ya Man United ikishinda 3-0 na Napoli ikashinda 2-0 na ilipata na ahueni ya mchezaji wa mpinzani wao kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya dakika 20. Hawajasafiri kutoka Urusi au Poland kwenda London. wametoka Manchester.”
“Sote tunajua changamoto za kuwa mchezaji ni kuwa na nguvu na kucheza michezo miwili au mitatu kwa wiki. Tukiona wachezaji wao walioko benchi, nina hakika kuna makocha wengine katika EPL wanaomtazama Pep na wanaona hakuna hoja hapa. Sikupenda mtazamo wake.”
Man City ilikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 32.8% tu, kiwango cha chini zaidi tangu Guardiola achukue usukani wa kuinoa mwaka 2016 na hii imekuwa tofauti na sifa yake ya kucheza soka la kuvutia.
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Guardiola, alicheka na kusema: “Lazima tuipe Arsenal sifa, kuzuia mara moja ndani ya miaka 10 si mbaya, sivyo? Lazima nijithibitishe tena kwa mkakati tofauti. Sasa nina timu ya mpito. Nilisema sijali kuhusu matokeo, nataka kuona roho ya kupambana ikirudi katika mazoezi na tufurahie. Baada ya hapo tutajadili mbinu za mchezo. Tulipoteza hilo msimu uliopita na tunalazimika kulirekebisha.”
“Wiki hii tumerudisha hali hiyo. Lazima tuendelee. Na kutoka hapo tutaendelea kujifunza mchakato, mbinu, ili tucheze vizuri na kushinda mechi huku tukiwa tunafurahia.”
Guardiola aliendelea kuchekesha akisema alitaka mpira uwe karibu na kipa wa Arsenal, David Raya, kuliko kipa wake Gianluigi Donnarumma.
“Niliteseka! Nilitaka mpira uwe karibu na Raya, sio Gigi, tulikuwa karibu sana kushinda.”
Arsenal iko pointi tano nyuma ya kinara wa ligi Liverpool, hali ambayo imezua presha kubwa kwa mashabiki ambao wanaona kocha wao Mikel Arteta hatoshi kuwapa taji wa Ligi Kuu England.