Keane awashangaa mastaa Man United

Muktasari:
- Man United imehamishia nguvu za msimu huu katika michuano ya Europa League, ambako itacheza na fainali na Tottenham - lakini kwenye Ligi Kuu England inashika nafasi ya 16 katika msimamo baada ya kupoteza mechi 18, ikiwamo kipigo cha 1-0 cha usiku wa Ijumaa kutoka kwa Chelsea.
MANCHESTER, ENGLAND: GWIJI wa Manchester United, Roy Keane amesema timu hiyo inatia aibu kwa rekodi za Ligi Kuu England msimu huu na kusema anaelewa sasa kwanini kocha Ruben Amorim alihitaji kujiunga na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Man United imehamishia nguvu za msimu huu katika michuano ya Europa League, ambako itacheza na fainali na Tottenham - lakini kwenye Ligi Kuu England inashika nafasi ya 16 katika msimamo baada ya kupoteza mechi 18, ikiwamo kipigo cha 1-0 cha usiku wa Ijumaa kutoka kwa Chelsea.
Wakati Amorim alipochukua mikoba ya kuinoa Man United kutoka kwa Erik ten Hag, Oktoba, timu hiyo ilikuwa nyuma kwa pointi sita tu kuifikia Top Four. Lakini, kwa sasa imeachwa pointi 27 nyuma kufikia nafasi hiyo ya kufuzu mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada kupoteza mechi nyingi za kiwango cha kutisha. Kocha Amorim amekuwa akibadilisha kikosi chake ili kujiandaa na fainali, lakini Keane bado anakwazwa na kiwango cha wachezaji wa Man United akiwaambia "hawapambani".
"Man United lazima ione aibu juu ya hili," alisema Keane na kuongeza: "Unachohitaji kutoka kwa wachezaji ni tabia. Ninachokiona, hawataki kupambana, hawahitaji ushindani. Unaweza kusamehe timu kupoteza, lakini unapomwona kocha anakuja kila wiki anakuna kichwa. Kichwa cha Amorim kimevurugwa kwa kuwa kocha wa Man United. Hii timu haijui jinsi ya kushindana. Hiki kitu sikielewi."
Kabla ya mechi ya Stamford Bridge, Man United ilipoteza mechi nne kati ya tano za mwisho kwenye Ligi Kuu England. Jambo hilo lilimfanya kocha Amorim kuwalaumu wachezaji kwamba hawana hofu kabisa ya kupoteza mechi, akisema: "Kama hatuhofii kupoteza mechi kama Man United basi hilo halitanitisha tena kwa sababu ni hatari kwa klabu kubwa kama hii kuwa na tatizo hilo."