Julian Nagelsmann aomba radhi, afafanua kauli yake dhidi ya Ireland Kaskazini
Muktasari:
- Nagelsmann alizua gumzo baada ya ushindi wa Ujerumani wa mabao 3-1 dhidi ya Ireland Kaskazini kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyochezwa Cologne mwezi Septemba 2025, aliposema kuwa kikosi cha Michael O'Neill kinacheza kwa kutumia mipira mirefu mingi na kwamba mtindo huo si wa kuvutia sana machoni.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, amesema hakuwa na nia ya kuidhalilisha timu ya Ireland Kaskazini, huku akiomba radhi iwapo kauli zake kuhusu mtindo wao wa uchezaji zilionekana kuwa na dhihaka.
Nagelsmann alizua gumzo baada ya ushindi wa Ujerumani wa mabao 3-1 dhidi ya Ireland Kaskazini kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyochezwa Cologne mwezi Septemba 2025, aliposema kuwa kikosi cha Michael O'Neill kinacheza kwa kutumia mipira mirefu mingi na kwamba mtindo huo si wa kuvutia sana machoni.
Kauli hizo zimeibuka tena kabla ya mechi ya marudiano ya Kundi A itakayopigwa leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 jijini Belfast, ambapo kocha wa Ireland Kaskazini, O'Neill, amejibu kwa kusema hata Ujerumani walitumia mipira mirefu mara kadhaa katika mechi ya awali, na kuongeza kuwa si kazi yake kujali kile wapinzani wao wanachokifikiria.
Alipoulizwa kuhusu kauli zake kupokewa kwa dharau, Nagelsmann amesema: “Sikumaanisha kudharau. Nilisema huenda isiwe ya kupendeza kuangalia, lakini jambo muhimu zaidi nililosema ni kwamba wanafanya vizuri. Wanacheza mipira mirefu kwa mpangilio fulani.
"Kuna hali ya kipekee ndani ya kikosi chao, na pia nilitaja kwamba ni vigumu sana kuwashinda, hawaruhusu mabao mengi na wanatengeneza nafasi nyingi kupitia mipira ya adhabu na kona kwa kutumia mtindo huo wa soka. Kwa hiyo kama mtu alihisi nimedharau, naweza kusema samahani. Lakini sikumaanisha hivyo."
Nagelsmann alianza mkutano wake na waandishi wa habari kwa kurudia maoni yake kwamba Ireland Kaskazini hupendelea kucheza mipira mirefu, lakini amekiri kuvutiwa na ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Slovakia, Oktoba 10, 2025, ushindi ambao umezifanya timu tatu za Ujerumani, Ireland Kaskazini na Slovakia kuwa na pointi sita kila moja kuelekea mechi za leo Jumatatu Oktoba 13, 2025.
“Waliweka shinikizo kubwa eneo la mwisho,” amesema Nagelsmann.
“Lazima utetee kwa umakini, mtu kwa mtu, kuzuia mipira ya krosi na adhabu. Kuna nafasi ya kushambulia kwa kushtukiza, lakini haitakuwa rahisi, tunapaswa kucheza vizuri sana ili kushinda mechi ya leo.”