Jezi mpya Man United kuzinduliwa wiki ijayo
Muktasari:
- Ingawa Man United haikuvaa mapema jezi yao ya sasa ya nyumbani mwishoni mwa msimu uliopita, jambo hilo la kuvaa jezi za msimu unaofuatia wakati msimu unaelekea kumalizika, si jipya na mara nyingi limekuwa na mafanikio makubwa kibiashara.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inatarajiwa kuvaa jezi yao mpya ya nyumbani ya msimu ujao katika mechi mbili za mwisho za msimu huu dhidi ya Nottingham Forest na Brighton.
Jezi hiyo itakayotumika msimu wa 2026-27, imetengenezwa na Kampuni ya Adidas na ina staili ya jezi maarufu za Man United za miaka ya 1970, ikiwa na kola yenye mistari pamoja na neno “United” lililoandikwa nyuma ya kola hiyo.
Ingawa Man United haikuvaa mapema jezi yao ya sasa ya nyumbani mwishoni mwa msimu uliopita, jambo hilo la kuvaa jezi za msimu unaofuatia wakati msimu unaelekea kumalizika, si jipya na mara nyingi limekuwa na mafanikio makubwa kibiashara.
Arsenal wamewahi kufanya hivyo hapo awali na hata mwaka jana waliivaa katika mechi zao za mwisho za ligi hiyo.
Wadau wengi wanaamini kuvaa jezi hiyo mapema ni njia ya kuongeza hamasa na matarajio ya mashabiki katika mechi kubwa kabla ya mapumziko marefu kuelekea ziara ya maandalizi ya msimu mpya.
Mbali ya kuachia jezi mpya, Man United pia itakuwa na mdhamini mpya katika jezi zao za mazoezi na kwa sasa kitengo chao cha biashara kinafanya mazungumzo na moja kati kampuni za kubahatisha (kubet).
Mkataba huo wa udhamini katika jezi za mazoezi unadaiwa utawapa mashetani hao wekundu takribani Pauni 18 milioni kwa mwaka.
Kampuni hiyo ya kubetisha inataka kuwekwa mbele ya jezi za mazoezi kwa sababu kuanzia msimu ujao, mamlaka zinazosimamia Ligi Kuu England hazitaruhusiwa tena kuweka kampuni za ubashiri mbele ya jezi za mechi.
Hata hivyo, marufuku hiyo haihusu jezi za mazoezi, hivyo, kampuni za ubashiri zimekuwa zikitafuta njia mbadala ya kufanya mikataba ya kibiashara na klabu kubwa za EPL na kwa sasa inaonekana fursa iko katika mazoezi.