Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jeraha la Jalen litakavyobadili maisha Knicks

NBA Pict

Muktasari:

  • Ingawa tukio hilo linachukuliwa kuwa la kawaida kwa wachezaji kutokana na migongano inayotokea uwanjani miongoni mwao, lakini limekuja katika kipindi ambacho Knicks ilihitaji uwepo wa Jalen kuliko wakati wowote ule kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi wa mara kwa mara kikosini.

LOS ANGELES, MAREKANI: NYOTA wa New York Knicks, Jalen Brunson anatarajiwa kukaa nje kwa wiki kadhaa baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati wa muda wa nyongeza kwenye mchezo wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) dhidi ya Los Angeles Lakers, ambao ulimalizika kwa Knicks kupoteza kwa pointi 113-109.

Ingawa tukio hilo linachukuliwa kuwa la kawaida kwa wachezaji kutokana na migongano inayotokea uwanjani miongoni mwao, lakini limekuja katika kipindi ambacho Knicks ilihitaji uwepo wa Jalen kuliko wakati wowote ule kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi wa mara kwa mara kikosini.

Mastaa wengine wanaoandamwa na majeraha madogo madogo mara kwa mara ni Josh Hart na Miles McBride sambamba na Cameron Payne huku ukuta wa timu hiyo ukiwa na uhakika wa mtu mmoja pekee - Delon Wright ambaye hana rekodi hiyo.

NB 01

Wachezaji wengine wanaoteswa na majeraha ya kila mara ni Yler Kolek, Mikal Bridges na Ariel Hukporti ilhali ubora wa Landry Shamet ukiwa wa kawaida na mara nyingi haanzi kikosini, jambo ambalo linampa wakati mgumu kocha Tom Thibodeau katika upangaji wa kikosi.

Ingawa Knicks katika msimamo wa NBA Kanda ya Mashariki inashika nafasi ya tatu kati ya timu 15 ikiwa na pointi 645, haiondoi ukweli kwamba kuandamwa na majeruhi wengi kikosini huenda kukaathiri mwenendo wa kikosi hicho katika ligi.

Kocha wa Knicks, Tom Thibodeau alithibitisha baada ya mchezo kwamba, Brunson alikuwa anafanyiwa vipimo na timu ya madaktari ili kubaini ukubwa wa jeraha lake.

“Ni jeraha la kusikitisha. Tunatarajia atakosekana kwa muda,” alisema mchezaji mwenzake, Josh Hart akionyesha wasiwasi juu ya athari za kutokuwepo kwa Brunson kwenye kikosi chao.

NB 02

Brunson, ambaye ni miongoni mwa wachezaji bora wa msimu huu wa NBA anashika nafasi ya saba katika orodha ya wafungaji bora akiwa na wastani wa pointi 26.3 kwa mchezo, huku pia akiwa wa nane kwa wastani wa pasi za kusaidia (assists) kwa mchezo akiwa na pointi 7.4.

Aliumia kwa kuangukia mguu wa mchezaji wa Lakers, Austin Reaves, baada ya kufanyiwa faulo alipokuwa akijaribu kupenya kuelekea kwenye kikapu akiwa amesalia na sekunde 1:24 kabla ya muda wa nyongeza kumalizika.

Baada ya kuanguka, Brunson alisaidiwa kusimama na wachezaji wenzake lakini alibaki uwanjani kupiga mikwaju miwili ya penalti na kusawazisha alama 107-107. Hata hivyo, mara baada ya penalti hizo, alitoka uwanjani na kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

NB 03

Katika mchezo huo, Brunson aling’ara kwa kuiongoza Knicks kwa kufunga pointi 39 na kutoa pasi 10 za usaidizi. Alihakikisha mchezo unaingia muda wa nyongeza baada ya kupiga mkwaju wa penalti wa pointi tatu wakati Lakers walipojaribu kurejea kutoka kwenye pengo la pointi mbili.

Thibodeau alimsifu Brunson kwa kiwango chake cha hali ya juu na moyo wa kupambana licha ya jeraha alilopata.

“Tunaweza kuzungumza kuhusu maumivu na matatizo ya kimwili, lakini kwa Brunson, uimara wake wa kiakili uko juu sana. Siwezi kushangaa kwa jinsi alivyopambana hadi mwisho. Alicheza kwa kiwango bora sana,” alisema Thibodeau.

Katika mchezo huo, Brunson alikuwa na ufanisi mkubwa kwa kupiga mashuti 13 kati ya 26 aliyojaribu kutoka uwanjani na kufunga mikwaju 12 kati ya 13 ya penalti alizopata.

Jeraha la Brunson limekuja katika kipindi kibaya kwa New York Knicks, kwani klabu hiyo ipo katika kipindi kigumu cha msimu ikipambana kubaki katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Kanda ya Mashariki ya NBA. Hili ni pigo kubwa kwa Knicks, hasa kutokana na ukweli kuwa wameanza safari yao ya mechi tano za mfululizo za ugenini kwenye ukanda wa Magharibi.

NB 04

New York Knicks, ambao wana rekodi ya ushindi 40 na vipigo 22, wanashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Kanda ya Mashariki. Wanaendelea kubaki Kusini mwa California ambapo wanakutana na Los Angeles Clippers usiku wa Ijumaa kabla ya kucheza dhidi ya Sacramento Kings Jumatatu usiku, Portland Trail Blazers Jumatano, na hatimaye Golden State Warriors Machi 15.

Kwa upande wake Karl-Anthony Towns, alisema kuwa licha ya jeraha la Brunson, wachezaji wengine wanapaswa kujitokeza na kuonyesha kiwango cha juu ili kufidia pengo lake.

“Hali ni ngumu, lakini hatuna muda wa kujutia. Tunapaswa kuwa na utayari wa kusonga mbele. Yeye (Brunson) ni sehemu muhimu ya timu yetu, lakini tumekuwa tukicheza kwa ari kubwa na tunapaswa kuendelea kufanya hivyo,” alisema Towns.

Kwa sasa, Knicks wanasubiri ripoti rasmi kutoka kwa madaktari kuhusu hali ya Brunson na muda ambao atakuwa nje ya uwanja. Ikiwa atakosekana kwa muda mrefu, basi Knicks italazimika kutafuta njia mbadala ya kujaza pengo lake, hasa katika safari yao ya mfululizo ya mechi za ugenini.

Jeraha la Brunson linaongeza orodha ya changamoto zinazokikabili kikosi cha Knicks katika kipindi hiki muhimu cha msimu, lakini bado wanabaki kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kufuzu kwa hatua za juu za michuano ya NBA mwaka huu. Itakuwa ni mtihani mkubwa kwa Thibodeau na kikosi chake kuona jinsi watakavyoweza kupambana bila mmoja wa wachezaji wao muhimu zaidi.