Jamal Musiala akaaa pazuri kwa mabao

Muktasari:
- Kwenye msimamo wa ufungaji bora kabisa fainali hizo, Musiala yupo kwenye namba moja, akiwa amefunga mara tatu kwenye dakika zake 29 tu alizokuwa uwanjani.
MIAMI, MAREKANI: STAA wa Bayern Munich, Jamal Musiala ameanza kwa kasi kubwa fainali za Kombe la Dunia la Klabu baada ya kuongoza vita ya ufungaji kufuatia kutikisa nyavu mara tatu katika michuano hiyo.
Nyota huyo aliingia kipindi cha pili kutokea benchi wakati Bayern iliposhusha kipigo cha mabao 10-0 dhidi ya Auckland City FC, akifunga hat-trick na kuwa kinara kwenye vita ya ufungaji bora kabla ya mechi za usiku wa Jumanne. Mechi hiyo ya Kundi C, iliifanya Bayern kuonyesha makali makubwa wakati ilipoichapa timu ya ridhaa ya kutoka New Zealand, ambapo mabao mengine ya wakali hao wa Ujerumani yalifungwa na Michael Olise, Kingsley Coman na Thomas Muller ambapo kila mmoja alifunga mara mbili uwanjani TQL, Cincinnati.
Kwenye msimamo wa ufungaji bora kabisa fainali hizo, Musiala yupo kwenye namba moja, akiwa amefunga mara tatu kwenye dakika zake 29 tu alizokuwa uwanjani.
Katika mechi za Jumanne, wachezaji waliokuwa wamefunga mabao mawili kila mmoja ni Olise, ambaye pia ana asisti mbili katika dakika 45 alizocheza, Coman mwenye asisti moja pia kwenye dakika 45 alizocheza na Muller, ambaye pia ana asisti moja katika dakika 90 alizocheza Bayern katika mchezo wa kwanza.