Ivory Coast ya Pacome na vigogo waliofuzu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Jambo hilo litafanya Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza kuwa na mchezaji kwenye fainali hizo za juu kabisa katika mchezo wa soka la ulimwengu.
SUPASTAA wa mabingwa wa kandanda nchini, Yanga, kiungo Pacome Zouzoua huenda akaiwakilisha Ligi Kuu Bara kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026 endapo atachaguliwa kuunda kikosi cha Ivory Coast kilichokata tiketi ya kushiriki michuano hiyo itakayofanyika huko Amerika Kaskazini.
Jambo hilo litafanya Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza kuwa na mchezaji kwenye fainali hizo za juu kabisa katika mchezo wa soka la ulimwengu.
Ivory Coast ilikata tiketi hiyo baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Kenya usiku wa Jumanne, shukrani kwa mabao ya Franck Kessie, Amad Diallo na Guela Doue, huku Pacome akiingia dakika 61 katika mchezo huo akimbadili winga wa zamani wa Arsenal, Nicolas Pepe.
Ivory Coast sasa inaungana na timu za Afrika Kusini , Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia, ambazo zimekamatia tiketi hiyo ya fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa ukanda wa Afrika.
Nchi za Ulaya bado hazikamilisha mchakato wao wa mechi za kufuzu, lakini tarifa imejionyesha huku England ikiwa taifa la kwanza kwenye bara hilo kunyakua tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
NCHI ZILIZOFUZU
Baada ya raundi iliyopita ya mechi za kufuzu, kumepatikana timu ambazo zimefanikiwa kuweka kibindoni tiketi ya Kombe la Dunia 2026, huku timu nyingine zikiendelea kupambana. Timu zilizofuzu kutoka mabara sita ni pamoja na;
Wenyeji: Canada, Mexico, United States
Asia: Australia, Iran, Japan, Jordan, Qatar, Saudi Arabia, Korea Kusini, Uzbekistan
Afrika: Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, South Africa, Tunisia
Ulaya: England
Oceania: New Zealand
Amerika Kusini: Argentina, Brazil, Colombia, Ecuador, Paraguay, Uruguay
TIMU ZINAZOWEZA KUFUZU
Kwa upande wa Afrika, timu za Cameroon, DR Congo, Gabon na Nigeria zitachuana kwenye mchujo kuwania nafasi ya mwisho ya kuwakilisha bara kwenye fainali hizo. Shirikisho la soka la Afrika (CAF) bado halijaweka hadharani tarehe ya kuchezwa kwa mechi hizo.
Kwa upand wa Asia, Falme za Kiarabu na Iraq zitachuana kuwania nafasi moja kwenye mechi ya mchujo, ambapo mechi mbili zitakazokutanisha timu hizo zitafanyika Novemba.
Huko Ulaya, timu 53 kati ya 54 zitachuana kuwania nafasi 16 za kufuzu fainali hizo za Kombe la Dunia, ambapo mechi za kwanza zitafanyika Novemba 18.
Amerika Kati na Kaskazini pamoja na Caribbean kutokana na mataifa mwenyewe kuchukua nafasi tatu, hivyo kuna nafasi tatu tu ndizo zilizobaki zinazoshindaniwa na timu za Bermuda, Costa Rica, Curacao, El Salvador, Honduras, Guatemala, Haiti, Jamaica, Nicaragua, Panama, Suriname na Trinidad & Tobago na kila kitu kitafanyika kwenye mechi za Novemba 18. Timu tatu zilizokuwa wa pili bora kwenye kila kundi zitachuana kwenye mchujo wa intercontinental, ambao utahusisha pia timu ya Oceania, New Caledonia.
Huko Amerika Kusini, Bolivia imefuzu kucheza mchujo wa intercontinental baada ya kukosa nafasi kwenye timu sita za juu zinazofuzu moja kwa moja fainali hizo za Kombe la Dunia kwa kutoka ukande huo.
MATAIFA MAKUBWA YATAKAYOKOSA
Peru na Chile ni miongoni mwa mataifa makubwa ya kutoka Amerika Kusini ambayo yameshindwa kukamatia tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2026 na kwamba hayatakuwapo kwenye fainali hizo sambamba na Venezuela. Huko Asia, China itasononeka kwa kukosa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2002, wakati Angola, Libya, Mali na Namibia hazitakuwapo kwenye fainali hizo za Amerika baada ya kushindwa kupenya Afrika.
Indonesia ilipambana walau kupata tiketi ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili, lakini imeshindwa kupenya huko AFC, licha ya timu hiyo kunolewa na kocha Patrick Kluivert.
LINI TIMU ZOTE ZITATHIBITISHWA?
Mchakamchaka wa kufuzu Ulaya utakwenda hadi Machi, mwakani wakati mchujo wa intercontinental utafika tamati, hivyo basi timu 48 zitakazocheza fainali zijazo za Kombe la Dunia hazitafahamika zote hadi kipindi hicho cha miezi mitatu kabla ya kuanza kwa fainali hizo. Machi 31, 2026, ndiyo zitachezwa mechi za mwisho za kufuzu. Droo ya fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 itafanyika Desemba 5 huko Washington, DC, huku fainali zenyewe mechi ya kwanza ikitarajiwa kufanyika Mexico City, Juni 11 na fainali itafanyika New Jersey, Julai 19.