Ishu ya Saka ndo hivyo, kukaa nje miezi miwili
Muktasari:
- Saka alipata maumivu kwenye mechi ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Crystal Palace na alikosa mechi ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ipswich Town, juzi Ijumaa usiku.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Arsenal, Bukayo Saka anatazamiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa misuli ya paja.
Saka alipata maumivu kwenye mechi ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Crystal Palace na alikosa mechi ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ipswich Town, juzi Ijumaa usiku.
Arsenal imeshathibitisha Saka atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nyingi na akizungumza kwenye mechi ya ushindi katika Ligi Kuu England dhidi ya Ipswich, kocha Mikel Arteta aliweka wazi muda ambao kikosi chake kitakosa huduma yake.
“Amefanyiwa upasuaji na kila kitu kimekwenda sawa, lakini bahati mbaya atakuwa nje kwa wiki nyingi sana,” alisema Arteta.
Kwenye hilo, Arteta aliongeza: “Nimesema wiki nyingi kwa sababu nadhani itakuwa zaidi ya miezi miwili. Sifahamu itakuwa muda gani. Hiyo itategemea na jeraha na kuanza kuwa kwenye uwezo wa kucheza.”
Arteta ana uhakika watacheza bila ya huduma ya Saka, ambapo mechi iliyopita, Gabriel Martinelli alicheza wingi ya kulia.