Budimir aipa Croatia pointi tatu muhimu, Panama ikiaga Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika Mechi hiyo ya kundi L iliyopigwa kwenye Uwanja wa BMO Field huko Toronto, Canada, Croatia ilipata bao hilo la dakika ya 54, la Budimir aliyemalizia pasi ya Josip Stanisic na kudumu hadi dakika 90 na kuitoa rasmi Panama licha ya kubakiwa na mechi moja mkononi.
TORONTO, CANADA: BAO la dakika ya 54 lililofungwa na nyota wa Croatia, Ante Budimir limetosha kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Panama ukiwa ni wa kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Croatia ilianza na kichapo cha mabao 4-2 dhidi ya England.
Katika Mechi iliyomalizika ya kundi L iliyopigwa kwenye Uwanja wa BMO Field, Toronto, Canada, Croatia ilipata bao hilo la dakika ya 54.
Budimir amefunga akimalizia pasi ya Josip Stanisic na kudumu hadi dakika 90, na kuitoa rasmi Panama licha ya kubakiwa na mechi moja mkononi.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Croatia katika Kombe la Dunia 2026 tangu ilipoichapa Morocco mabao 2-1 katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu iliyopigwa Qatar, Desemba 17, 2022.
Timu hizo zilianza kampeni ya Kombe la Dunia kwa vichapo ambapo Croatia ilichapwa na England mabao 4-2, huku Panama ikashangazwa na Ghana kwa kufungwa bao 1-0.
Matokeo hayo yanaifanya Croatia kufikisha pointi tatu katika kundi L ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya England na Ghana zenye nne kila moja, huku Panama ikiburuza mkiani bila pointi baada ya kuchapwa mechi zote mbili.
Croatia inashiriki mara saba michuano ya Kombe la Dunia tangu ilipoanza 1998 huko Ufaransa na kushangaza mashabiki wengi wa soka duniani baada kumaliza ikishika nafasi ya tatu.
Katika michuano ya mwaka 1998, aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Davor Suker aliyetamba Real Madrid na Sevilla za Hispania na pamoja na Arsenal ya England, alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia akimaliza na mabao sita.
Mafanikio makubwa kwa Croatia ni ya Kombe la Dunia 2018 lililofanyika Russia, ambapo ilifika fainali kwa mara ya kwanza, japokuwa ilichapwa na Ufaransa mabao 4-2, Julai 15, 2018 na kumaliza ikiwa nafasi ya pili.
Katika Kombe la Dunia 2022 Qatar, Croatia iliendeleza kiwango bora na kuishia nusu fainali baada ya kuchapwa na mabingwa Argentina mabao 3-0, Desemba 3, 2022, japo ilishika mshindi wa tatu kwa kuifunga Morocco mabao 2-1, Desemba 17, 2022.
Kwa upande wa Panama hii ni mara ya pili katika historia ya timu hiyo kushiriki Kombe la Dunia baada ya mara ya kwanza kuandika historia iliposhiriki mwaka 2018, kwenye fainali hizo zilizofanyika Urusi na kikosi hicho kuchapwa mechi zote tatu za kundi G.
Katika kundi hilo la G, Panama iliburuza mkiani baada ya kuchapwa mechi zote tatu nyuma ya vinara Ubelgiji iliyokuwa na pointi tisa, ikifuatiwa na England iliyoshika ya pili na pointi sita na Tunisia iliyomaliza ya tatu na pointi zake tatu.
Licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika historia yake, ila mchezaji wa Panama, Felipe Baloy aliandika rekodi mpya ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza la Kombe la Dunia kwenye kichapo cha kikosi hicho cha mabao 6-1, dhidi ya England, Juni 24, 2018.