Isak aanza kuwapa joto mabosi wa Newcastle Utd
Muktasari:
- Fundi huyu ambaye vigogo wengi barani Ulaya wanaitaka huduma yake, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na mabosi wa Newcastle wanataka kumwongeza ili kuzima kabisa tamaa za timu zinazomhitaji.
MSHAMBULIAJI wa Newcastle na timu ya taifa ya Sweden, Alexander Isak mwenye umri wa miaka 25, anataka mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki ili kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye timu hiyo.
Fundi huyu ambaye vigogo wengi barani Ulaya wanaitaka huduma yake, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na mabosi wa Newcastle wanataka kumwongeza ili kuzima kabisa tamaa za timu zinazomhitaji.
Katika dirisha hili Liverpool ndio inaonekana kuwekeza nguvu zaidi kuhakikisha inaipata saini yake lakini bado inaonekana kuwa ngumu kwani Newcastle haiko tayari kumwachia na hata ikiamua kufanya hivyo ni pale tu timu inayotaka huduma yake itakapotoa zaidi ya Pauni 130 milioni, kiasi kinachoonekana kuwa kikubwa sana.
Kocha Eddie Howe amewaambia mabosi wa Newcastle kwamba Isak ni sehemu muhimu sana ya mipango yake kuelekea msimu ujao na asingependa kuona anauzwa.
Hivi karibuni kocha huyu alilazimika kumweka Isak nje katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Celtic kutokana na tetesi zinazoendelea kwa sasa.
Liverpool ipo tayari kuvunja beki kwa ajili ya kuhakikisha staa huyu anatua katika dirisha hili na ipo tayari hata kuachana na staa wao Darwin Nunez na yeye ndio awe mbadala wake.
Taarifa za ndani zinafichua kwamba Newcastle iltaka kimpa mshahara wa Pauni 200,000 ikiwa atakubali kusaini mkataba mpya. Kiasi hicho ni ongezeko la Pauni 70,000.
Granit Xhaka
GRANIT Xhaka ameripotiwa kukubali ofa ya kujiunga na Sunderland, katika dirisha hili na sasa timu hiyo itatakiwa kufanya mazungumzo na Bayer Leverkusen kuhusu ada ya kiungo huyo wa kati wa Uswisi mwenye umri wa miaka 32. Awali, ilidaiwa kuwa Xhaka huenda angetua Saudi Arabia ambako aliwekewa ofa nono lakini amegeuzia gia angani na kukubali ofa ya Sunderland kwani anaona bado anahitaji kucheza soka la kiushindani.
Yoane Wissa
BRENTFORD imekataa ofa ya kwanza ya Pauni 30 milioni kutoka klabu ya Newcastle inayohitaji saini ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwenye umri wa miaka 28, Yoane Wissa katika dirisha hili.
Mabosi wa Brentford wapo tayari kumwachia fundi huyu lakini kwa kiasi cha pesa ambacho kitakuwa ni zaidi ya Pauni 40 milioni. Hadi kufikia sasa tayari Wissa na wawakilishi wake wameshafanya makubaliano binafsi na Newcastle.
Rasmus Hojlund
ATALANTA na Lazio zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Denmark, Rasmus Hojlund mwenye umri wa miaka 22. Timu zote zinataka kumsajili mshambuliaji huyu ambaye haonekani kuwa sehemu ya mipango ya Ruben Amorim kwa msimu ujao. Atalanta ndio inaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuipata saini yake katika dirisha hili.
Renato Veiga
ATLETICO Madrid imeanza mazungumzo na Chelsea kuhusu uwezekano wa kuipata saini ya beki wa kati wa timu hiyo, Renato Veiga, ili kumsajili katika dirisha hili. Kwa mujibu wa mwandishi nguli wa habari za usajili, Fabrizio Romano, Chelsea ipo tayari kumuuza staa huyu wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 21, lakini inahitaji takribani Pauni 35 milioni. Atletico haipo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa.
Adam Aznou
EVERTON inafanya kila linalowezekana ili kuipata huduma ya beki wa kushoto wa Bayern Munich mwenye umri wa miaka 19, Adam Aznou. Staa huyu wa kimataifa wa Morocco ameonyesha kutamani sana kutua Everton kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha Bayern na ndio anaona ni nafasi pekee ya kucheza kwani mbali ya ongezeko la mshahara Everton pia imemhakikishia kumpa nafasi ya kucheza EPL.
Jhon Arias
WOLVES iko karibu kukamilisha usajili wa winga wa Colombia, Jhon Arias mwenye umri wa miaka 25 kutoka Fluminense, pamoja na beki wa kulia Mhispania Marc Pubill mwenye umri wa miaka 22 kutoka Almeria wote katika dirisha hili. Arias na Pubill wote wameshafanya makubaliano binafsi na mabosi wa Wolves kilichobaki ni kumalizana.
Dan Sinate
MANCHESTER United inamfuatilia beki wa kushoto wa Angers, Dan Sinate, ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Mali ya vijana chini ya miaka 20. Hata hivyo, itakapofanikiwa kumsajili haitomchukua moja kwa moja badala yake itamwacha hadi mwakani kabla ya kumjumuisha katika kikosi.