Inter yaibana City, Inzaghi alia na mastaa wake
Muktasari:
- Inter ilikuwa wageni wa Man City kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi na kulazimisha suluhu, huku kocha huyo akisema kuwa sababu ya matokeo hayo ni mastaa wake kupoteza nafasi nyingi za wazi.
Milan. Kocha wa Inter Milan Simone Inzaghi, amesema anaridhishwa na mwenendo wa timu yake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kulazimisha sare dhidi ya Manchester City.
Inter ilikuwa wageni wa Man City kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi na kulazimisha suluhu, huku kocha huyo akisema kuwa sababu ya matokeo hayo ni mastaa wake kupoteza nafasi nyingi za wazi.
Inter ilionyesha kiwango cha juu kwenye Dimba la Ettihad na kuizuia timu hiyo ambayo iliwachapa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023.
Mastaa wa Inter, Matteo Darmian na Henrikh Mkhitaryan walipoteza nafasi nyingi za wazi, huku pia staa wa City Ilkay Gundogan, akipoteza nafasi mbili za wazi za kufunga mabao.
Hata hivyo, matokeo hayo yamemfanya kocha huyo kuwa wa pili kwenye historia kutoka suluhu na Man City ikiwa chini ya Pep Guardiola kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa kwenye Uwanja wa Etihad.
"Vijana wangu walicheza vizuri sana, tunafahamu ubora wa wapinzani wetu lakini tulifanya kila jambo kuhakikisha kuwa tunatimiza malengo yetu, nafikiri tulikuwa tunaweza kuwaadhibu kama tungetumia nafasi zetu vizuri.
"Kwenye eneo letu la ushambuliaji, nafikiri tulikuwa tunaweza kufanya jambo, tulitakiwa kuhakikisha tunatumia vizuri nafasi tulizozipata kwa kuwa ngumu kupatikana mara mbili," alisema Simon ndugu na Philipo Inzaghi.
Kocha huyo amesema kwa sasa wanahamishia nguvu zao kwenye mchezo wa dabi kati yao na AC Milan kwenye ligi ya Serie A, Jumapili ijayo.
Kwa upande wa Guardiola, alisema anaamini kuwa vijana wake watabadilika kwenye michezo ijayo kwa kuwa hawakuonyesha uwezo mzuri wakiwa nyumbani, hata hivyo amesema bado hajafahamu kama kiungo wake Kelvin de Bruyne atakaa nje kwa muda gani baada ya kuumia kwenye mchezo huu.
Matokeo mengine ya mechi hizo za kwanza za Ligi ya Mabingwa hatua makundi yalishuhudia PSG ikiichapa Girona 1-0, Celtic ikishinda 5-0 dhidi ya Slovan, Dortmund wakiibuka na ushindi wa 5-0 dhidi ya Club Brugge, Bologna na Shakhtar mechi ikimalizika kwa suluhu.