Inter Milan yatwaa taji la 20 Serie A

MILAN, ITALIA. INTER Milan imecheza soka la kibabe ikiichapa mahasimu wao AC Milan mabao 2-1 na kutwaa taji lao la 20 la Serie A huku ikiwa bado na mechi tano mkononi.

Staa Francesco Acerbi alitumia uzembe wa mabeki wa AC Milan kuifungia Nerazzurri bao la mapema ndani ya dakika 20 za mchezo. Na baada ya kupoteza nafasi kadhaa za kufunga, Inter ilifunga bao la pili, shukrani kwa kazi nzuri kabisa ya Mfaransa, Marcus Thuram kwenye dakika ya 49.

Fikayo Tomori aliifungia AC Milan bao la kujifariji dakika za mwisho kabla ya vuta nikuvute iliyotokea mwishoni iliyowahusisha mastaa Theo Hernandez, Denzel Dumfries na Davide Calabria na wote walionyeshwa kadi nyekundu.

Lakini, mwisho wa mechi, Inter ndiyo iliyopata ushindi dhidi ya mahasimu wao hao na kunyakua taji lao la kwanza la Scudetto tangu msimu wa 2020-21.


Kwa Simone Inzaghi, alisherehekea taji lake la kwanza la Serie A akiwa kocha, akiongeza pale kwenye mataji matatu ya Coppa Italia na matano ya Italian Super Cup ambayo amebeba katika kipindi chake cha ukocha.

Wakitambua ushindi unawapa taji, Nerazzurri ilihitaji dakika 18 tu kufunga bao la kuongoza huko San Siro.

Kona fupi ya Federico Dimarco ilikutana na Benjamin Pavard, ambaye alipiga mpira matata kabisa kwa Acerbi, aliyesukumia nyavuni na kuandika bao lake la tatu msimu huu.

Kinara wa mabao wa Serie A, Lautaro Martinez alishindwa kuongeza idadi yake ya mabao baada ya kupaisha mpira mbele ya goli la AC Milan kutokana na pasi matata kabisa ya Dimarco.



Baada ya kubanwa, hatimaye kilifika kipindi ambacho AC Milan nao walionyesha anaweza kufunga baada ya Rafael Leao kupiga shuti kwa guu la kushoto, lakini kipa Yann Sommer alikuwa imara na kuudhibiti mpira huo.

Inter nusura ifunge bao la pili baada ya Nicolo Barella na Thuram kugongeana pasi, lakini straika huyo wa Ufaransa alipiga nje ya goli la Mike Maignan.

Baada ya hapo kosakosa zilikuwa nyingi kabla ya Thuram kuifungia bao la pili Inter na hapo kuwahakikishia kwamba pointi tatu zinawahusu.
Kipigo hicho cha AC Milan kimezidisha presha kwa kocha wao Stefano Pioli, ambaye alitupwa nje ya Europa League na kuchapwa kwenye Derby della Madonnina.