Huko Liverpool pancha kibao!

Muktasari:
- Majogoo hawa walitolewa na Paris Saint-Germain katika mzunguko wa 16 wa Ligi ya Mabingwa na wakapoteza mchezo wa fainali ya Carabao Cup dhidi ya Newcastle.
LIVERPOOL, ENGLAND: HIVI karibuni hali ya Liverpool inaonekana kuwa sio nzuri kutokana na matokeo ambayo imekuwa ikiyapata katika michuano mbalimbali.
Majogoo hawa walitolewa na Paris Saint-Germain katika mzunguko wa 16 wa Ligi ya Mabingwa na wakapoteza mchezo wa fainali ya Carabao Cup dhidi ya Newcastle.
Hivi vilikuwa ni vipigo viwili mfululizo vya kushtua ndani ya siku sita, ambavyo vimetibua mwendo wa kibabe wa vinara hawa wa Ligi Kuu England ambao walianza msimu kwa kishindo.
Liverpool inapambana kushinda taji lake la pili katika kipindi cha miaka mitano, lakini hofu imezidi kutanda kutokana na idadi kubwa ya majeraha ambayo wachezaji wao muhimu wameyapata na idadi hiyo inazidi kuongezeka.
Kabla ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, Liverpool tayari ilikuwa inawakosa mastaa wake muhimu kama Trent Alexander-Arnold ambaye aliumia kifundo cha mguu kwenye mchezo dhidi ya PSG, Joe Gomez anayetarajiwa kuukosa msimu mzima baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Plymouth Februari mwaka huu.
Pia walikuwa wakiwakosa Harvey Elliott, Conor Bradley na Tyler Morton lakini sasa idadi imezongezeka baada ya Ryan Gravenberch naye kuumia akiwa katika mazoezi ya timu ya taifa ya Uholanzi.
Kiungo huyu ameanza karibia mechi zote za Liverpool kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kukosekana kwake katika eneo la kiungo kunaweza kuwa pigo kubwa kwa kocha Arne Slot.
Hakuna majibu yaliyotolewa juu ya ukubwa wa jeraha lake ingawa ripoti zinaeleza staa huyu alitengeneza pacha nzuri kati yake na Alexis Mac Allister, atafanyiwa vipimo zaidi jijini Liverpool ili kuona ukubwa wa tatizo ingawa majogoo wana matumaini makubwa kwamba ataiwahi mechi ijayo ya Aprili 2 dhidi ya Everton.