Hossam Hassan atisha watu mtoano AFCON 2025
Muktasari:
- Kocha Hassan, ameshinda mataji matatu ya Afcon kipindi akiwa mchezaji wa Misri, akifanya hivyo mwaka 1986, 1998 na 2006.
CASABLANCA, MOROCCO: KOCHA Mkuu wa Misri, Hossam Hassan amesema kucheza mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kila baada ya miaka miwili huzivutia ligi za Ulaya, huku akisisitiza kikosi chake kipo imara kukabiliana na timu yoyote kwenye hatua ya 16 bora huko Morocco.
Misri ilitoka 0-0 na Angola mjini Agadir na hivyo kutopoteza mechi yoyote kwenye Kundi B na kuongoza ikiwa na pointi saba, ikimaliza juu ya Afrika Kusini, ambayo imeshika namba mbili baada ya kukusanya pointi sita kufuatia ushindi wa 3-2 dhidi ya Zimbabwe.
“Kwa mtazamo wangu ni vyema Kombe la Mataifa ya Afrika lingekuwa linafanyika kila baada ya miaka miwili badala ya minne,”€ amesema Hassan.
“Hii ingekuwa na faida kubwa kwenye ligi za Ulaya.”
Shirikisho la soka la Africa (CAF) lilitangaza wiki iliyopita kwamba mashindano ya Afcon kwa miaka ijayo itaanza kufanyika kila baada ya miaka minne, ikiachana na utaratibu wa kila baada ya miaka miwili ulioanzishwa tangu mwaka 1957.
Kwa kuongoza kundi, Misri itaendelea kubaki Agadir hadi hapo itakapocheza mechi yake ya mtoano kwenye hatua ya 16 bora, Jumatatu ijayo.
“Tupo tayari kupambana na timu yoyote itakayokuja mbele yetu kwenye raundi ya 16 bora, hatua inayo ni ngumu sana na mashindano yatakuwa na upinzani. Tutafanyia kazi juu ya maandalizi ya mechi ijayo na kurekebisha makosa,” amesema Hassan.
Misri ilipuumzisha wachezaji wake kadhaa katika mechi ya mwisho ya kundi, akiwamo Mohamed Salah na Omar Marmoush ili kuwapa mapumziko ya kujiandaa na mechi ya mtoano.
Kocha Hassan, ameshinda mataji matatu ya Afcon kipindi akiwa mchezaji wa Misri, akifanya hivyo mwaka 1986, 1998 na 2006.