Hii kitu ya Palmer ngoja tuone mwisho
Muktasari:
- Hata hivyo, lisemwalo noi kwamba nyota huyo wa kimataifa wa England hana utulivu kwa sababu anawakosa marafiki zake wa nyumbani na hivyo kwa sasa akilini mwake anaweza kuvutiwa na mpango wa kurudi Manchester City au kwenda Manchester United, klabu aliyokuwa akiishabikia alipokuwa mtoto.
LONDON, ENGLAND: KWA maelezo ya kocha wa Chelsea, Liam Rosenior ni kwamba kiungo Cole Palmer anafurahia maisha Stamford Bridge.
Hata hivyo, lisemwalo noi kwamba nyota huyo wa kimataifa wa England hana utulivu kwa sababu anawakosa marafiki zake wa nyumbani na hivyo kwa sasa akilini mwake anaweza kuvutiwa na mpango wa kurudi Manchester City au kwenda Manchester United, klabu aliyokuwa akiishabikia alipokuwa mtoto.
Palmer, mwenye umri wa miaka 23, alionekana kutokuwa katika hali yake ya kawaida wakati wa mchezo dhidi ya Brentford wikiendi iliyopita, ambapo alikataa kushangilia penalti yake ya dakika za mwisho na akaelekea moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya mechi kumalizika.
Hata hivyo, Rosenior anasisitiza kuwa Palmer alikuwa amekatishwa tamaa na matatizo ya majeraha yanayoendelea, si kwa sababu hana furaha kwenye timu.
Kocha mkuu wa Chelsea alisema: “Nimezungumza na Cole mara nyingi na anaonekana kuwa ana furaha sana kuwa hapa. Ana furaha sana kuwa hapa. Yeye ni sehemu kubwa ya mipango yetu ya muda mrefu.
“Ni mchezaji wa kipekee. Kila mchezaji hupitia nyakati ngumu katika taaluma yake, hasa linapokuja suala la majeraha. Lakini kazi yangu na kazi ya klabu ni kumfikisha katika hali ambayo anaweza kucheza kwa kiwango anachotaka mara kwa mara. Kulikuwa na hali ya kukerwa katika mechi dhidi ya Brentford, si kwa sababu hakuwa na furaha hapa, bali kwa sababu hakuweza kucheza vizuri. “Alikuwa anaumia. Hakuweza kutoa kiwango alichotaka kwa ajili ya klabu. Ni kijana mzuri na mchezaji wa kiwango cha juu, lakini ni lazima tumlinde kwa njia sahihi.”
Rosenior alimwacha Palmer nje ya kikosi katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki dhidi ya Pafos, kutokana na maumivu madogo ya paja.
Hata hivyo, bosi huyo wa Chelsea anatambua umuhimu mkubwa wa mchezaji wake namba 10 katika matumaini ya The Blues msimu huu.
Rosenior alisema: “Cole akiwa fiti kabisa na katika ubora wake, simchukui mchezaji yeyote duniani katika nafasi yake badala yake. Nimezungumza naye mara nyingi na anaonekana kuwa na furaha sana kuwa hapa. Kazi yangu ni kumuunga mkono. Sio mimi peke yangu bali wafanyakazi, madaktari, wachezaji wenzake ili kuhakikisha hahisi kukata tamaa.
“Ni jambo zuri kuwa anakasirika kidogo, maana inaonyesha anataka kufanya vizuri kwa klabu. Lakini sitaki ajilazimishe kucheza hadi kufikia maumivu, hasa tukiwa Januari. Hilo halina maana. Tuna wachezaji kadhaa tunaopaswa kuwalinda kwa njia tofauti, badala ya kuwalazimisha kucheza bila kuwa tayari.
“Nina imani na kikosi. Nimekuwa nikifanya mzunguko wa wachezaji na nitaendelea kufanya hivyo, kwa sababu nataka tuwe kwenye michezo mikubwa na mashindano makubwa mwishoni mwa msimu.”
Palmer pia anaweza kuwa na wasiwasi kuhusu mashindano makubwa zaidi ya Kombe la Dunia 2026 yatakafanyika majira ya kiangazi mwaka huu.
Nyota huyo wa Chelsea bado hajachezea England chini ya Thomas Tuchel kutokana na majeraha, na mechi za kirafiki za Machi zitakuwa za mwisho kabla Tuchel hajatangaza orodha ya awali ya wachezaji kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Rosenior alisema: “Ukweli kwa Cole ni kwamba, akicheza katika kiwango chake, ataingia kwenye kikosi. Ni rahisi sana. Akicheza kwa kiwango chake cha asili akiwa fiti, sina shaka kuwa kila kitu anachokitaka katika taaluma yake kitamjia. Kazi yetu kwa sasa ni kumfikisha katika hali ambayo anaweza kwenda na kufurahia kucheza uwanjani.”
Wakati huo huo, Chelsea imepigwa faini ya Pauni 150,000 baada ya chupa ya maji kurushwa kutoka eneo lao la benchi la ufundi kuelekea kwa wachezaji na benchi la Aston Villa katika mechi yao ya Desemba 27 mwaka jana. Tukio hilo lilichunguzwa na klabu pamoja na FA, lakini hakuna aliyeweza kubainishwa kama mhusika aliyerusha chupa hiyo, ambayo ilipita karibu na kichwa cha mchezaji mmoja aliyekuwa kwenye benchi la Aston Villa.
Chupa hiyo ilirushwa baada ya mshambuliaji Ollie Watkins kufunga mabao mawili yaliyowapa Aston Villa ushindi wa kushtukiza dhidi ya The Blues.