Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hata tabasamu la mke wa Xabi Alonso linahitajika Real Madrid

Muktasari:

  • Akiwa kama mchezaji, Alonso na Madrid wana historia ya kipekee, ndio klabu aliyoichezea michezo mingi na kwa muda mrefu zaidi, na kubwa kuliko ndipo sehemu aliposhinda taji pekee la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).

Hadi sasa Xabi Alonso ndiye anatajwa kurithi mikoba ya Carlo Ancelotti ndani ya Real Madrid baada msimu huu kumalizika, anarejea nyumbani Santiago Bernabeu kama kocha mwenye mafanikio na baba wa watoto watatu.

Akiwa kama mchezaji, Alonso na Madrid wana historia ya kipekee, ndio klabu aliyoichezea michezo mingi na kwa muda mrefu zaidi, na kubwa kuliko ndipo sehemu aliposhinda taji pekee la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).

Mwezi mmoja kabla ya kujiunga na Madrid akitokea Liverpool FC mwaka 2009, kiungo huyo alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, Nagore Aranburu, na kwa sasa wana watoto watatu pamoja ambao ni Jontxe (2008), Ane (2010) na Emma (2013).

Uhusiano wa Alonso na mkewe Nagore, umekuwa chanzo cha utulivu na furaha katika maisha yake yote ya soka kama mchezaji na sasa akiwa kama kocha aliyebeba matumaini makubwa ya Madrid ambao msimu huu wamepoteza michezo yote minne ya El Clasico dhidi ya mahasimu wao Barcelona.

Nagore, mwanamitindo, muigizaji na mbunifu wa mitindo kwa miaka mingi, ni mwanamke ambaye Alonso alikutana naye wakati wa ujana wake alipokuwa akiichezea klabu yake ya utotoni, Real Sociedad alipodumu kati ya mwaka 2000 hadi 2004.

Wawili hawa ambao ni wenyeji wa eneo la Basque nchini Hispania, kipindi uhusiano wao unaanza, licha ya maisha yao yenye shughuli nyingi na ratiba za kuchosha, bado walikuwa na uhakika wa kupata wakati wa kukaa pamoja na kuzifikia ndoto zao.

Siku ya harusi yao Nagore alimzawadia Alonso saa ya mkononi aina ya IWC Ingenieur yenye thamani ya Euro 10,500, ni zawadi yenye maana kubwa kwa mchezaji huyo aliyeshinda Kombe la Dunia 2010, michuano iliyofanyika Afrika Kusini.

“Zawadi hii inawakilisha ukweli kwamba nimepata mwanamke ambaye anafikiria kuhusu mimi, juu ya kile ninachopenda, na utu wangu,” alisema Alonso na kuongeza:

“Siivai sana saa, ni katika hafla maalum tu. Kwangu, kila wakati maalum lazima uhusishwe na saa, na kila ninapoiwasha kuna jambo..., nakumbuka tulivyoshinda UEFA 2005 tukiwa na Liverpool au Kombe la Dunia 2010 tukiwa na Hispania.”

Kwa miaka yote uhusiano wao umesalia kuwa msingi wa maisha yao, kila mmoja amedhihirisha na kujitoa ipasavyo ili kusonga mbele kama familia yenye lengo moja la kuacha alama kwa kila kazi ya mikono yao.

Kati ya simulizi za kufurahisha kuhusu Nagore, ni kipindi akiishi huko Merseyside, England na kufanya kazi kama mhudumu wa mapokezi katika hoteli huku mumewe wakati huo akiichezea Liverpool, mabingwa wa Ligi Kuu England (EPL) mara 20.

Aliyekuwa mchezaji wa Liverpool, Peter Crouch alimuona Nagore akiwa kazini kwake na kuvutiwa naye kutokana na uzuri wake bila kujua ni mpenzi wa mchezaji mwenzake kutokea viunga vya Anfield.

“Wakati wa kusaini Liverpool nilikaa katika hoteli ya Hope Street, pale mapokezi kulikuwa na msichana mzuri sana, sikuweza kuamini kabisa alivyokuwa akinitazama na kutabasamu kila wakati,” alisema Crouch.

Alipofika mazoezini, Crouch aliwasimulia wachezaji wenzake kuhusu urembo wa msichana huyo (Nagore) akisema ni wa kushangaza, mwenye nywele nyeusi na muonekano wa Kihispania, hivyo anahisi kama kwake tayari amefika.

Jamie Carragher, mchezaji wa zamani wa Liverpool, aliwaita wachezaji wachache waandamizi na kumwambia Crouch arudie kile alichosema kuhusu msichana huyo. Ndipo akaja kuelezwa huyo ni mpenzi wa Alonso na anafanya kazi hiyo ili kujifunza lugha ya Kiingereza.

Kwa miaka yote, Nagore na watoto wake, wamemfuata Alonso kila sehemu ambapo kazi yake ilimpeleka, wamekuwa wote kuanzia San Sebastian hadi Liverpool, Madrid, Munich na kisha kurejea tena kwao Basque, na baadaye Leverkusen alikoandika historia.

Ikumbukwe Oktoba 2022, Alonso alianza kukinoa kukosi cha Bayer 04 Leverkusen, na msimu uliopita akawapa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1904.

Furaha aliyowapa Leverkusen, ndicho kitu ambacho Real Madrid wanakitaka baada ya kudhalilika vya kutosha kwa kufungwa mechi zote nne za kimashindano na ya tano ya kirafiki walipokutana na mahasimu wao FC Barcelona msimu huu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 11.1, Alonso alichapisha picha akitabasamu pamoja na familia yake kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Leverkusen na kuandika, ‘timu yangu’ kisha kumalizia emoj ya upendo.

Hiyo ilikuwa ishara ya kuthamini mchango wa familia yake ikiwa ni muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Bundesliga kufuatia ushindi wa mnono wa mabao 5-0 mbele ya Werder Bremen kwenye Uwanja wa BayArena.

Na hiki ndicho wanakihitaji Real Madrid kutoka Alonso baada ya msimu huu kushindwa kutetea taji la UEFA kufuatia kuadhibiwa vikali na Arsenal, huku wakiendelea kuburuzwa na FC Barcelona katika msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Laliga).

Lakini Alonso naye anahitaji tabasamu la mkewe na familia yake yote kwa ujumla ili kufanikisha kile ambacho Madrid wanataka kutoka kwake, na mtihani wake wa kwanza unatajwa kuwa ni Kombe la Dunia la Klabu 2025, michuano itakayofanyika kuanzia Juni.