HAMNIWEZI: Guardiola awazodoa, Ferguson, Abramovich

Kocha wa Barcelona Pep Guardidola akipongezana na kocha wa Real Madrid Jose Mourinho akiwa kulia
MADRID, HISPANIA HATIMAYE Udinese imekubali kupokea kitita cha Pauni 33 milioni kutoka Barcelona, sasa winga Alexis Sanchez atatua katika kikosi kinachonolewa na Pep Guardiola wakati wowote wiki hii. Barcelona imezipiga teke klabu nyingi za Ulaya ambazo zilikuwa zikimwania mchezaji huyo kwa karibu. Chelsea, Manchester City, Real Madrid na Manchester United zilikuwa zikiwania saini ya mchezaji huyo lakini sasa zitatakiwa kutafuta wachezaji wengine. Mchezaji huyo raia wa Chile mwenye umri wa miaka 22 sasa yupo nchini kwake akijiandaa na michuano ya Copa America itakayofanyika Argentina mwezi ujao lakini atalazimika kwenda Hispania kutia saini mkataba mpya wiki hii. "Udinese imekubali kumuuza Sanchez kwenda Barcelona kwa pauni 33 milioni," liliripoti gazeti la La Tercera. Sanchez, ambaye anafahamika kama 'Kid Marvel', alifunga mabao 12 msimu uliomalizika na kuisaidia Udinese kumaliza Ligi ya Serie A katika nafasi ya nne, hivyo itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. El Mercurio limeripoti kuwa Sanchez amepewa ruhusa na kocha wa timu ya taifa ya Chile, Claudio Borghi aende kufanyiwa vipimo vya afya Alhamisi wiki hii. Kwa maana hiyo mchezaji huyo atakosa mechi ya kirafiki dhidi ya Paraguay wiki hii. Lakini Sanchez atakuwemo katika kikosi cha Chile wakati kitakaposhuka dimbani kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Estonia huko Santiago Jumapili wiki hii. Sanchez alisajiliwa katika kikosi cha Udinese mwaka 2006 kwa ada ya Pauni 1.7 milioni akitokea Cobreloa.Lakini alitolewa kwa mkopo kwenda Colo-Colo na baadaye River Plate mwaka 2007.