Hali ya kiusalama Mashariki ya Kati yatishia mechi za Nigeria kufutwa
Muktasari:
- Hali hii inatokana na mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyofanywa kwa pamoja na Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanzia jana Jumamosi, Februari 28, 2026, yaliyosababisha vifo vya viongozi wa juu wa Iran, akiwemo Kiongozi Mkuu Ali Khamenei.
MECHI za kimataifa za kirafiki kati ya timu ya taifa ya Nigeria maarufu Super Eagles dhidi ya Iran na Jordan zilizopangwa kuchezwa mwezi huu, huenda zikafutwa kutokana na hali mbaya ya kiusalama Mashariki ya Kati.
Hali hii inatokana na mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyofanywa kwa pamoja na Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanzia jana Jumamosi, Februari 28, 2026, yaliyosababisha vifo vya viongozi wa juu wa Iran, akiwemo Kiongozi Mkuu Ali Khamenei.
Nigeria inatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki katika mashindano ya nchi nne (Four-Nation Tournament) jijini Amman, Jordan.
Taifa hilo la Afrika Magharibi linatarajia kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Iran (Team Melli), iliyopangwa kufanyika Ijumaa, Machi 27, 2026, huku mpinzani wa pili akitarajiwa kuwa wenyeji Jordan, Machi 31, 2026.
Kocha wa Nigeria, Éric Chelle, ambaye aliteuliwa Januari 2025, anatarajiwa kukiongoza kikosi chake kwenye mechi hizo za kimataifa za kirafiki, ambazo zinatajwa kuwa shakani kuchezwa, kufuatia hali ya kiusalama huko mashariki ya kati.
SABABU ZA TISHIO LA KUFUTWA
Mashambulizi ya Kijeshi: Operesheni za kijeshi za Marekani na Israel zimesababisha machafuko makubwa. Iran imelipiza kisasi kwa kushambulia maeneo ya Marekani na Israel nchini Jordan, Qatar, UAE, Syria, na Saudi Arabia.
Usalama wa Wachezaji: Mashirikisho ya soka yamehoji usalama wa wachezaji nchini Jordan, huku safari nyingi za ndege zikisitishwa na anga la mataifa kwa nchi za Kiarabu kufungwa.
Hali ya Iran: Shirikisho la Soka la Asia (AFC) tayari limeshairisha mechi za klabu ukanda wa Magharibi, na uongozi wa soka wa Iran umetilia shaka ushiriki wao hata katika Kombe la Dunia la 2026 kutokana na hali ya vita.