Haaland ataja magwiji anaowaiga kupiga mabao
Muktasari:
- Straika huyo wa Manchester City anajiandaa kwa ushindani mkali dhidi ya Arsenal katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, aliwataja washambuliaji wengine ambao amekuwa akijifunza kutoka kwao ambao Sergio Aguero, Zlatan Ibrahimovic na Jamie Vardy.
MANCHESTER, ENGLAND: STRAIKA la mabao, Erling Haaland amefichua supastaa Robin van Persie ni mmoja wa washambuliaji aliowafuatilia kwa karibu kwa ajili ya kujifunza na kukuza kipaji chake.
Straika huyo wa Manchester City anajiandaa kwa ushindani mkali dhidi ya Arsenal katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, aliwataja washambuliaji wengine ambao amekuwa akijifunza kutoka kwao ambao Sergio Aguero, Zlatan Ibrahimovic na Jamie Vardy.
Hata hivyo, fowadi huyo wa Norway amewapita wote hao kwa kuwa mchezaji aliyefikisha kwa haraka mabao 100 kwenye Ligi Kuu England.
Akiwa mfuatiliaji mkubwa wa soka la Ligi Kuu England hata kabla ya kuhamia nchini humo, amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kutoka kwa magwiji hao na Haaland amesema: “Nilimtazama sana Zlatan nilipokuwa mdogo, ilikuwa nzuri kumuangalia. Aguero nilimtazama kwa sababu alikuwa Man City, bila shaka. Van Persie alipokuwa kwenye Ligi Kuu England, mguu wa kushoto na mabao ya ajabu. Nakumbuka msimu mmoja alifunga takribani mabao 38, ulikuwa mwaka wa kipekee kwake.
“Hata Vardy, mbio alizokuwa akikimbia zilikuwa za kushangaza kuona, hivyo nilitazama washambuliaji wengi. Mambo mengi niliyogundua nilikuwa mzuri kwao, namna ya kufunga mabao inaweza kuwa rahisi, unachukua vitu vidogo kutoka kwa washambuliaji tofauti halafu unaenda na mtindo wako mwenyewe. Nilipokuwa mdogo nilitaka kuwa bora zaidi lakini pia kufurahia soka langu. Nilikuwa na kipaji kizuri na watu wazuri walionizunguka, jambo lililonipa mtazamo sahihi wa kufanya mazoezi.”
Haaland alifikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu England wakati alipofunga dhidi ya Fulham mwezi Desemba na aliifikia rekodi hiyo katika michezo 13 pungufu kuliko aliyekuwa mmiliki wa rekodi hiyo awali, Alan Shearer.
Haaland amesema: “Ni jambo la kujivunia kuwa kileleni mwa orodha. Mabao 100 katika Ligi Kuu England si jambo rahisi. Ni kitu spesho kufanya hivyo kwa muda mfupi kiasi hiki.”